SERIKALI YATANGAZA KUZIMA LAINI ZA SIMU ZILIZOSAJILIWA KWA UONGO SIKU YA WAPENDANAO

 

Waziri wa Habari, Teknolojia ya habari na Mawasiliano Nape Nnauye akizungumza na Waandishi wa habari leo Dodoma kwenye ukumbi wa habari -Maelezo.


Na Dotto Kwilasa, DODOMA.

WAZIRI wa Habari, Teknolojia ya habari na Mawasiliano Nape Nnauye amesema siku moja kabla ya siku ya wapendanao (Valentine's day) Wizara hiyo kupitia mamlaka ya mawasiliano inatarajia kuzima laini zote za simu ambazo zimesajiliwa kwa njia ya udanganyifu.

Waziri Nape amesema hayo leo Jijini hapa wakati akizungumza na Waandishi wa habari na kueleza kuwa jumla ya laini zinazo tarajiwa kuzimwa ni milioni 2.3 ifikapo February 13 mwaka huu ikiwa ni maandalizi ya kuingia siku ya wapendanao February 14,2023.

Amesema ,Sekta ya mawasiliano inakuwa sana na kutokana na utandawazi huo zipo line zinazotumika vibaya na kuwasababishia watu kuibiwa hivyo kutokana na zoezi hilo itasaidia kupunguza utapeli mtandaoni.

"Kuna zaidi ya laini million 60 zilizosajiliwa lakini kati ya hizo ni laini milioni 58 tu ambazo zimehakikiwa huku laini  zinazotarajiwa kuzimwa ni laini milioni 2.3 ambazo hazijahakikiwa,tunafanya utambuzi huu  kumlinda mtumiaji mtandao ili kuwa salama,"amesema Nape.

Katika hatua nyingine Waziri huyo ameeleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan haridhishwi na hali ya Waandishi wa habari nchini hivyo kutaka tathimini ya kina kufanyika kuhufu namna ya kuondoa changamoto zilizopo.

Kutokana na hayo amesema Wizara yake imefanya mazungumzo na kuunda Kamati ya watu tisa kutathmini 
hali ya vyombo vya habari kiuchumi  na kiutendaji.

Amewataja wanakamati hao kuwa "Mwenyekiti wa Kamati Tido Mhando ambaye ni Mtendaji Mkuu Azam Media Group,Katibu wa Kamati Gerson Msigwa Mkurugenzi idara ya habari Maelezo na msemaji wa Serikali huku wajumbe wakiwa ni Bakari Machumu, Joyce Mhavile, Richard Mwaikenda, Dk.Rose Rueben,Kenneth Simbaya , Sebastian Maganga na Jackline Woiso".

Waziri Nape amefafanua kuwa Kamati hiyo itafanya kazi ya kuchakata taarifa kwa kina na kutumia nafasi hiyo kuwaomba Waandishi wa habari kutoa  ushirikiano na  kutoa maoni Kwa njia ya mtandao bila kulazimu mtu kusafiri na kwamba itafanya kazi ndani ya muda wa miezi mitatu ili kukwamua tasnia ya habari.

"Vile vile Kamati itafanya kazi ya kukusanya  taarifa za waandishi wa habari walioajiriwa,Wenye mikataba ,vipato vyao ,wawakikishi mikoani ikiwa ni pamoja na  kupendekeza njia bora za kukabiliana na changamogo hizo,"amesisitiza.

Kwa upande wake Msemaji wa Serikali Gerson Msigwa  ametumia nafasi hiyo kuwashukuru wanahabari kwa kufanya kazi kwa bidii kipindi chote cha mwaka uliopita huku akiwata kuendelea kuchapa kazi kwa uzalendo na kujitolea kwa manufaa ya Taifa.

"Mwaka jana tulishuhudia uzalendo wa hali ya juu,hakukuwa na habari zinazotugawa wala chuki na huu ndiyo uzalendo tunaoutaka,nichukue fursa hii  kuwataka Waandishi wa habari kuendelea kufanya kazi kwa kufuata misingi na maadili ya uandishi wa habari,"amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments