CCM YAAGIZA WALIMU WAPEWE VISHIKWAMBIChama Cha Mapinduzi (CCM) kimetoa wiki moja kwa Wizara ya Elimu kuanzia leo Januari 20, 2023 kuhakikisha vishikwambi vilivyotolewa na serikali kwa ajili ya walimu vinawafikia walengwa.

CCM imesema imepokea malalamiko ya kutotekelezwa kikamilifu kwa maelekezo ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuhusu ugawaji wa vishikwambi hivyo.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam , Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi Ndugu Sophia Mjema, alisema wakati akizundua ugawaji wa vishikwambi hivyo Novemba mwaka jana, Waziri Mkuu Majaliwa aliagiza kuhakikisha vifaa hivyo vinakwenda kwa walengwa.

"Ulitengwa muda maalumu wa kutolewa kwa vishikwambi hivi ambao ulikuwa unaishia Januari 15, mwaka huu, lakini Chama kimepokea malalamiko kwamba hadi leo kuna baadhi ya makundi hayajapata hivyo vishikwambi. Lakini pia kuna baadhi ya wilaya hawajagawa kabisa vishikwambi hivyo.

"Kuna maeneo mengine unakuta walimu wako 10 na wote wanahitaji na wanastahili kupata, lakini unakuta vishikwambi vinatoka vinane wawili wanaachwa.

"Chama kinatoa maelekezo, kinaielekeza wizara husika (Wizara ya Elimu) kuhakikisha zoezi hili linakamilika na walengwa wote wanaostahili kuhakikisha wameipata vishikwambi hivyo, lakini siyo hivyo tu bali pia wahakikishe malalamiko haya hayapo na wasimamie zoezi kuona makundi yaliyopaswa kupewa yanafikiwa na wale ambao hawajapata wapate. Baada ya wiki moja tupate taarifa zoezi hili limekwendaje," amesema.

Mjema alisema kutolewa kwa vishikwambi hivyo ni mwendelezo wa jitihada za serikali kuwawezesha na kuwajengea uwezo walimu kuwa na vitendea kazi na kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Katika kuendelea kuwawezesha walimu kuwa na vitendea kazi na kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji Septemba 15, mwaka jana kwamba vishkwambi vilivyotumika wakati wa sensa ya watu na makazi Agosti 23, mwaka 2022 vitatagawiwa kwa walimu wote baada ya shughuli hiyo kumalizika.


Naibu waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Juma Kipanga alisema jumla ya vishikwambi vilivyotumika wakati wa sensa ya watu na makazi 6,600 kwa upande wa Zanzibar na 293,400 Tanzania Bara.

Aidha, alisema wizara hiyo imeongeza vishikwambi zaidi ya laki moja hivyo kufanya idadi hiyo kutosheleza.

Walengwa na ugawaji huo ni walimu wote, baraza la mitihani, wadhibiti ubora, wakufunzi wa vyuo vya ualimu, vyuo vya maendeleo ya jamii na vyuo vya ufundi pamoja na waratibu elimu kata na maafisa elimu wilaya na mkoa.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

Post a Comment

Previous Post Next Post