WAZAZI WAPELEKA WATOTO KUOSHWA DAWA ZA MVUTO WA MAPENZI


Na Nyamiti Alphonce Nyamiti.

Wananchi wa kata ya Usule wilaya ya Shinyanga Mkoani Shinyanga wamekiri watoto wao kuwaosha dawa ya mvuto wa mapenzi 'Nsamba' kwa Waganga wa kienyeji ili kupata mwanaume mwenye mali anayekubalika kwenye familia husika.


Wameyabainisha hayo kupitia mdahalo uliofanyika katika Shule ya Msingi Usule ulioendeshwa na Mratibu wa mradi wa kupinga vitendo vya ukatili Dhidi ya wanawake na watoto bi. Mariam Maduhu kupitia shirika la Rafiki SDO kwa ufadhili wa shirika la Women Fund Tanzania (WFT).


"Nilishuhudia mimi kwa jirani yangu alimpeleka mtoto kuoshwa dawa hizi hatimaye mganga akamuoa mwenyewe", Alisema Anna Kadala


"Mimi nawashauri Waganga wa kienyeji dawa hizi wawaogeshe watu wanaohitaji kwa hiyari tena wenye umri wa kuolewa", alisema Mageshi Malimi.

Hata hivyo baadhi yao wamesema imani hiyo haina ukweli ndani yake isipokuwa ni mbinu za kiudanganyifu zinazofanywa na baadhi ya Waganga wakienyeji kujipatia fedha kutokana na Waganga hao kuwa makuwadi wa wanaume waliokosa wanawake wa kuoa kwa muda mrefu.


Bw Mhoja Masolwa ni miongoni mwa waganga wa kienyeji wa kata ya Usule ameonyesha kukerwa na baadhi ya Waganga wanaotumia kivuli cha kuagua watu na badala yake wanaingiza vitendo vya utapeli na ukatili.


"Nikweli dawa hiyo ipo na inafanya kazi vizuri kama ilivyo tu dawa ya kumpatia mtu utajiri ni kweli mwandishi wa habari kwani hujawahi kusikia mtu ameenda kutafuta mali kwa mganga na akafanikiwa? Isipokuwa tu mimi nasikitika kwa Waganga wenzangu kuwaosha dawa hizi watoto wadogo unakuwa hutendi haki", alisema Mhoja


Kwa upande wao Meneja wa shirika la Rafiki SDO, Asante Nselu na Mratibu wa mradi huo, Mariam Maduhu wamesema lengo la mradi huo ni kuhakikisha jamii inaelewa maana na vitendo vya ukatili Ili jamii yenyewe iweze kujilinda dhidi ya vitendo hivyo hasa kwa makundi ya wanawake na watoto.


Maduhu ameongeza kuwa kupitia mradi huo kwenye kata ya usule wamefanikiwa kwaasilimia kubwa kuweza kuifumbua jamii hasa wanawake katika kuripoti moja kwa moja kwenye vyombo husika pindi tu wanapogundua viashiria ama uwepo wa ukatili wanaofanyiwa wao ama mtu mwingine.


"Kupitia elimu tunayoitoa watu wa usule hususani wanawake sàsa wanao mwamko mkubwa kuhusiana na matukio ya ukatili sasa baadhi yao wanao uwezo wa kujisimamia na kujiokoa kwenye dimbwi la ukatili", alisema Maduhu


Akizungumzia juu ya uwepo wa vitendo vya ukatili Afisa mtendaji wa kata hiyo , Nshimba Waziri alisema wanaendelea kutoa elimu ya ukatili na kuwachukulia hatua za kisheria wale ambao wanaotekeleza matukio ya ukatili.


Vile vile Waziri amelipongeza shirika la Rafiki SDO kwa kuendesha programu mbalimbali ndani ya kata hiyo ikiwemo utoaji wa elimu ya kupinga Ukatili imesaidia kuiamsha jamii na kujitambua.


"Sisi kama serikali tumekuwa tukisimamia sheria kwa mjini wa katiba na niwaombe tu wananchi kujiepusha na vitendo vya ukatili kwani elimu imeshatolewa sana na inaendelea kutolewa", alisema Waziri.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments