ZIARA YA MTENDAJI MKUU TARURA YALETA FARAJA KWA WANANCHI- KALIUA

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor H. Seff ameleta faraja kwa wakazi wa Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora baada ya kutembelea barabara ya Mpandamlowoka-Mwaharaja na Kazaroho-Mpandamlowoka zenye urefu wa Km 90 na kusema hatua za matengenezo zinaendelea ili kuhakikisha wananchi wanafikia huduma za kijamii.


Mtendaji Mkuu ametembelea barabara ya Mpandamlowoka-Mwaharaja na Kazaroho-Mpandamlowoka ikiwa zimepita siku chache baada ya Waziri wa Nchi-OR TAMISEMI Mhe. Angellah Kairuki kumuagiza afike eneo hilo ili kukagua na kutafuta namna ya kutatua changamoto za barabara hizo.


“Nimefika eneo hili ili kujionea namna hali ilivyo ili kuchukua hatua za haraka na za muda mrefu kwa ajili ya kutatua changamoto ya usafiri kwa wakazi wa maeneo haya ili waweze kufikia huduma za kijamii na kuendelea na shughuli zao za kichumi. Nimekuta mkandarasi anaendelea na kazi lakini analegalega, hivyo nimetoa maagizo kwa Meneja wa TARURA Wilaya amsimamie mkandarasi kwa karibu ili barabara ziweze kupitika kabla ya mwezi Desemba kuisha ”, alisema Mhandisi Seff.


Pia, Mhandisi Seff ameziomba Mamlaka za Serikali za Mitaa mkoani Tabora kuendelea kutoa ushirikiano hasa wakati wa kuandaa Bajeti ili kuhakikisha barabara zenye changamoto ambazo ni muhimu zinapewa kipaumbele kwa kutengewa fedha ili ziweze kufanyiwa matengenezo na kupunguza adha kwa wananchi.


Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Mhe. Paul Chacha amemshukuru Mtendaji Mkuu wa TARURA kufika eneo hilo na kuona hali halisi na kueleza umuhimu wa barabara hizo kwa kuwa zinaunganisha barabara kuu ya kwenda Kahama ambayo inawasaidia wananchi kusafirisha mazao yao hasa mpunga na pia barabara zote mbili zinapita maeneo ya mbuga.


Kwa upande wao wananchi wa Kaliua wameushukuru uongozi wa TARURA kwa kutembelea eneo hilo na kuleta suluhisho la adha kubwa walizokuwa wanazipata.


“Tunaishukuru Serikali kwa kutuona wananchi wa maeneo haya, kwa kweli adha tunazopata ni kubwa sana kwenye usafiri wananchi tunalazimika kutumia gharama kubwa ya usafiri ambapo nauli kwa sasa ni shilingi elfu 35 hadi shilingi elfu 40, sasa tunafurahi serikali imetuona na tunaomba ituboreshee barabara hizi”, alisema Ndg. Philbert Agostino mkazi wa Kaliua.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post