DKT. HUSSEIN MWINYI ATAKA KISWAHILI KIKUZE UCHUMI


Katibu mtendaji wa Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) Dkt. Bi. Mwahija Juma(mwenye mtandio rangi ya machungwa) akimuonyesha vitabu vilivyoandaliwa na baraza hilo ,Rais Dkt. Hussein Mwinyi.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi akihutubia katika kongamano la 6 la Baraza la Kiswahili Zanzibar( BAKIZA).
NA ELISANTE KINDULU, WETE-PEMBA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesisitiza kuwa wataalamu wa lugha ya Kiswahili waitumie lugha hiyo katika kukuza uchumi.


Dkt. Mwinyi aliyasema hayo alipokuwa akifungua kongamano la 6 la kimataifa lililoandaliwa na baraza la kiswahili Zanzibar( BAKIZA) katika ukumbi wa baraza la wawakilishi Mjini Wete hivi karibuni.


Dkt. Mwinyi alisema lugha ni hazina na ajira inayoweza kukuza uchumi kwa wasomi kuitumia katika uandishi wa vitabu, uandishi wa habari, uhariri, uchapaji, huduma za tafsiri , ukarimalimani pamoja na utunzi wa kazi za Sanaa na ubunifu.


Rais Mwinyi aliwaambia washiriki wa kongamano hilo kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaweka mkazo maalumu katika vyuo ili kupata wataalamu wabobezi.

"Nawapongeza BAKIZA kwa kuleta kongamano lenu hapa Pemba. Nawashauri muendelee kufanya tafiti mbalimbali ili kukuza lugha ya Kiswahili , lakini pia muendelee kuibua vipaji vya watunzi wa fasihi na kazi za Kiswahili", alisema.


Aidha Dkt. Mwinyi aliagiza kuwa Wizara na taasisi zote kutekeleza maagizo ya kutumia lugha ya Kiswahili katika nyaraka , mikataba, mabango, vifungashio na nembo.


Dkt. Mwinyi aliwasihi pia waandishi wa habari kuzingatia matumizi fasaha ya Kiswahili na kuitumia lugha hiyo bila ya kuchanganya na lugha nyingine katika kazi zao za uandishi na utangazaji.


Kongamano hilo lilikuwa la siku mbili lilijadili mada mbalimbali kutoka kwa washiriki ndani ya Zanzibar, Tanzania bara na nchi za Afrika Mashariki na Marekani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments