SERIKALI YADHAMILIA KUTEKELEZA KWA VITENDO MPANGO WA KUBORESHA MAZINGIRA YA BIASHARA


Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kutekeleza kwa vitendo Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (MKUMBI) ili kuvutia waweklezaji nchini.

Mhe. Kijaji ameyasema hayo tarehe 17 Novemba, 2022 alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Ulaya Nchini Tanzania Mhe. Manfredo Fanti aliyeambatana na ujumbe wake.

Mhe. Dkt. Kijaji amemshukuru Mhe. balozi Fanti kwa ushirikiano endelevu uliopo baina ya Tanzania na Umoja wa Ulaya katika utekelezaji wa miradi mbalimbali na kumhakikishia kuwa Tanzania itaendelea kuboresha Mazingira ya Biashara kupitia MKUMBI ambapo sheria na kanuni mbalimbali zimeboreshwa ama kufutwa ili kurahisisha ufanyaji Biashara Nchini Tanzania.

“Mazingira ya kufanya Biashara yameboreka zaidi kwani hivi karibuni tunaenda kuzindua mfumo wa dirisha moja la huduma kwa wawekezaji wa Ndani na Nje ya Nchi ili kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali ikiwemo maombi ya leseni, vibali, hati na kurahisisha malipo ndani ya muda mfupi. Amesema Dkt. Kijaji.

Balozi wa Umoja wa Ulaya Nchini Tanzania Mhe. Manfredo Fanti amesema kuwa Mazingira ya Biashara Nchini Tanzania yamezidi kuboreka siku hadi siku na Nchi za Umoja wa Ulaya zimedhamiria kuja kuwekeza Tanzania katika sekta mbalimbali.

Mhe. Balozi Fanti ameongeza kuwa kutokana na Tanzania kuanzisha na kutekeleza MKUMBI, Mpango huo utaenda kuchapishwa katika tovuti ya Umoja wa Ulaya na kupitia Kongamano la Uwekezaji linaloenda kufanyika Mwezi Februari 2023 litawaunganisha wafanyabiashara wa Nchi za Umoja wa Ulaya na Tanzania na utapelekea kuongezeka kwa uwekezaji baina ya Nchi hizi mbili

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments