Mwanaume mmoja huko Donholm nchini Kenya amefariki dunia baada ya majambazi kumpiga risasi mara nne, na kumpokonya begi waliofikiri lina pesa, ila kupata limejaa vikombe vya karatasi.
Nicodemus Munyasya mwenye umri wa miaka 38, alikuwa ametoka kwenye benki kupeleka hundi, wakati wanaume wawili waliojihami walimfuata kwa kutumia boda boda na kumpiga risasi.
Kwa mujibu wa ripoti kwenye jarida la the Daily Nation, polisi wanashuku kwamba majambazi hao walikuwa wanamjua mwendazake, wakati alipomshambulia eneo la Savannah na kumuitisha begi hilo.
"Alikuwa amebeba begi la mizigo lililokuwa na vikombe vya karatasi, wakati majambazi hao walipodhania zilikuwa ni pesa,” taarifa ya polisi ilisema.
Munyaswa alipigwa risasi mara tatu mguuni na mara moja kwenye kifua. Mwili wake umepelekwa kuhifadhiwa katika chumba cha maiti kwenye Hospitali ya Mama Lucy.