MWANAFUNZI WA SHULE YA MSINGI MZEE ZAIDI AFARIKI DUNIA


Priscilla Sitienei amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 100.

MWANAFUNZI mkubwa zaidi wa elimu ya msingi nchini Kenya, Priscilla Sitienei amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 100.


Sitienei alikuwa maarufu kwa jina la Gogo ambalo kwa lugha ya asili ya kabila la Kalenjin linamaanisha ‘bibi’.


Mjukuu wa Sitienei, Sammy Chepsiror amelieleza gazeti la The Standard la nchini humo kuwa ‘Gogo’ amefariki dunia akiwa katika hali ya utulivu mbele ya baadhi ya wanafamilia.


Hadithi yake ya kujiunga na elimu ya msingi akiwa na umri wa miaka 94 iliwavutia watengeneza filamu wa Ufaransa waliotengeneza filamu ya Gogo, ambayo ilimpa fursa “Gogo” kukutana na mke wa rais wa Ufaransa, Brigette Macron.Priscilla Sitienei akiwa na wanafunzi wenzake enzi za uhai wake

Mmoja wa waandishi wa filamu hiyo, Patrick Pessis ametuma salamu za rambirambi kufuatia msiba huo akiandika katika ukurasa wa Twitter “ujumbe kuhusu elimu kwa wasichana unaendelea kubaki”.


Gogo Sitienei alijiunga na shule ya watoto ya Vision Preparatory School akijiunga na darasa la wanafunzi ambao ni sawa na vilembwe wake alipoamua kurejea shule akiwa na miaka 90 baada ya kufanya kazi ya ukunga wa jadi kwa zaidi ya miongo miwili.


Sitienei hakufanikiwa kujiunga na shule alipokuwa mdogo lakini serikali ya Kenya ilipoamua kuweka unafuu wa gharama za elimu ya msingi mwaka 2003 ilimhamasisha Gogo na wazee wengine kurejea darasani.


Mwaka 2015 Gogo aliiambia BBC kuwa analenga kuwahamasisha watu wazima kurejea shule “Wananiambia wao ni wakubwa [na hawawezi kurudi shuleni kusoma]” nitawajibu, “Mimi ni mzee [zaidi yao] na ninasoma darasani hivyo ni lazima warudi kusoma”. Alinukuliwa na BBC.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments