WAFANYAKAZI TASAF WAKUSANYA MIL.3.2/- KUSAIDIA WAGONJWA OCEAN ROAD

Ofisa Ustawi wa Jamii wa Taasisi ya Saratani Ocean Road, Justine Chambo akiwashukuru na kujibu baadhi ya maswali ya wafanyakazi wa TASAF waliotoa msaada wa vifaa na dawa kwa wagonjwa waliolazwa kwenye taasisi hiyo.

Baadhi ya wafanyakazi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya kukabidhi msaada huo kwa wagonjwa waliolazwa kwenye Taasisi ya Saratani Ocean Road jijini Dar es Salaam leo Oktoba 15,2022.

**********************

Na Irene Mark

WAFANYAKAZI wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), wametoa msaada wa dawa na vifaa mbalimbali vyenye thamani ya sh. 3,247,800 kwa ajili ya wagonjwa waliolazwa katika Taasisi ya Saratani Ocean Road jijini Dar es Salaam.

Msaada huo umetolewa leo Oktoba 15,2022 na baadhi ya wafanyakazi ambao walipata fursa ya kuwaona, kuzungumza na kuwapa msaada wagonjwa waliolazwa kwenye taasisi hiyo.

Akizungumza baada ya kukabidhi msaada kwa wagonjwa, mwakilishi wa wafanyakazi wa TASAF, Marylinda Meero amesema wafanyakazi wanaguswa na matatizo ya wananchi hivyo wamejichangisha fedha hizo ili kuwasaidia wenye uhitaji zaidi.

Meero amesema jumla ya fedha iliyopatikana iligawanywa kwenye manunuzi ya vifaa na dawa za wagonjwa kama walivyoelekezwa na uongozi wa Taasisi ya Saratani Ocean Road.

“Ni wafanyakazi tumeguswa tukaona ni vema kuja hapa kwa kuwa wapo wahitaji ambao hawana uwezo ndio maana tumejichangisha tukapata sh. 3,247,800.

“...Tumefuata ushauri wa hospitali tumenunua vifaa ambavyo ni sabuni za unga, miche, dawa za miswaki, miswaki yenyewe, maji ya kunywa, malapa na ‘dypers’ za wakubwa.

“Jumla ya sh. 627,000 tumenunua vifaa na iliyobaki sh. 2,600,800 tumenunua dawa mbalimbali kwa ajili ya wagonjwa wetu na sisi wachache tumewawakilisha wenzetu wengi kuja hapa leo.

“Tunaushukuru uongozi wa Taasisi ya Ocean Road na wafanyakazi wenzangu kwa msaada huu na muda wao kwa kweli tumefarijika kuwashika mkono wagonjwa tunawaombea kwa Mungu awaponye,” amesema Meero.

Ofisa Ustawi wa Jamii wa Taasisi ya Ocean Road, Justine Chambo amewashukuru wafanyakazi wa TASAF kwa ukarimu na kuwakumbuka wagonjwa huku akiwaombe heri na afya njema wote walioshiriki kwa michango na muda wao.

Chambo amesema msaada huo umewafariji wagonjwa na kuwapa tabasamu licha ya maumivu makali wanayopitia.

Kwa mujibu wa Chambo, asilimia 70 ya matibabu yote mpaka chakula katika taasisi hiyo hutolewa bure hivyo wanapopata msaada kutoka kwa jamii wanashukuru na wanapata moyo zaidi wa kuwahudumia wagonjwa hao.

“Tunapotembelewa kama hivi na sisi watoa huduma tunafurahi na kufarijika pia kuona kwamba jamii inatambua mchango wetu. Mungu awabariki na msichoke kutusaidia,” amesema Chambo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post