SERIKALI YATAKA TSC KUSHUGHULIKIA TATIZO LA UTORO KWA WALIMU.

 
Katibu wa TSC ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume hiyo,Paulina Nkwama .

Naibu Waziri  TAMISEMI anayeshugulikia Afya,Dk.Festo Dugange.

Na Dotto Kwilasa, DODOMA.

TUME ya utumishi wa Walimu nchini (TSC)imetakiwa kuwachukulia hatua za kinidhamu walimu ambao wamekuwa wakifanya vitendo viovu ambavyo ni kinyume na maadili ya taaluma yao ikiwa ni pamoja na kuangalia changamoto inayo sababisha kuongezeka kwa  utoro kwa Walimu nchini.

Naibu Waziri  TAMISEMI anayeshugulikia Afya,Dk.Festo Dugange ametoa maagizo hayo leo Jijini Dodoma wakati akifungua Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Utumishi wa Walimu TSC na kusema kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa ikiwajali watumishi hasa Walimu Kwa kuwapa stahiki zao.

Amesema Serikali  imeweza kuwapandisha vyeo zaidi ya Walimu laki mbili kwa Mwaka 2021/2022 ikiwa ni pamoja na kulipa stahili mbalimbali za madai na kwamba itaendelea kuongeza Bajeti katika kada hiyo ili kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Dkt.Dugange amesema  "Naitaka Tume hii ya Utumishi wa Walimu kuendelea kuwaelimisha pia walimu kutambua wajibu wao ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi kwani jumla ya walimu 7,579 ni watoro sawa na asilimia 66.5 ,"amesema.

Pia aliitaka Tume ya Utumishi ya Walimu kutowafumbia macho walimu wasiozingatia maadili ya kazi ambapo jumla ya walimu 11,396 wamechukuliwa hatua mbalimbali za kinidhamu kutokana na makosa mbalimbali yaliyofanywa na walimu.

“Naagiza Waajiri na Mamlaka ya Nidhamu kuchukua hatua mara moja pindi kunapokuwa na uthibitisho wa Mwalimu kukiuka Sheria, Kanuni, Taratibu na Maadili ya Kazi ya Ualimu na ya Utumishi wa Umma kwa ujumla,” amesema  

Kwa Upande wake Katibu wa TSC ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume hiyo,Paulina Nkwama ameishukuru Serikali kwa kushughulikia madai mbalimbali na kueleza mashauri ya walimu yanaendelea kushughulikiwa.

Amesema tume hiyo kwa kushirikiana na OR – TAMISEMI imefanya tathmini kwa kutumia Mfumo wa TAMISEMI ujulikanao kama School Information System (SIS) na  kubaini kuwa, mahitaji ya walimu kwa Shule za Msingi ni 298,313 huku waliopo ni 173,591.

"Bado pia kuna upungufu ni 124,732 sawa na 58%. Aidha, mahitaji ya walimu Shule za Sekondari ni 175,592, waliopo ni 84,700 na upungufu ni 90,892 sawa na 48%. Taarifa hiyo iliwasilishwa kwa Katibu Mkuu OR – TAMISEMI na kuwezesha walimu 9,800 kuajiriwa mwezi Juni, 2022”amesema.

Amefafanua kuwa Tume hiyo pia iliratibu na kushughulikia masuala ya utumishi ya Walimu ambapo Walimu 43,322  waliajiriwa; Walimu 41,675 (96.2%) kati ya walioajiriwa, walisajiliwa ; Walimu 33,129 (76.5%) walithibitishwa kazini; Walimu 250,905 na walipandishwa cheo ni  Walimu 22,456.

"Walimu waliobadilishwa cheo baada ya kujiendeleza kielimu ni 30,773, waliandikiwa vibali vya kustaafu kazi; Mafao ya Walimu 2,282 yanayohusu Pensheni, Mirathi na Mikataba yalishughulikiwa na Tume na kulipwa na Hazina,amesema na kuongeza;. 

Tume ilitoa uamuzi wa mashauri ya nidhamu 11,396 (98.8%) kati ya 11,529 yaliyoanzishwa na katika makosa yaliyotendwa, kosa la utoro limeongoza kwa kuwa na walimu 7,579 (66.5%), makosa mengine tofauti na utoro ni 33.5%  ambayo ni pamoja na kughushi vyeti 1,438, mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi 328, ulevi 89 na uzembe 56,"amesema.

Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Walimu nchini TSC limekutana kwa lengo la kujadili Kuhusu wajibu na Haki za wafanyakazi ikiwemo hoja mbalimbali za Wajumbe zitakazowasilishwa toka katika Kila Kanda.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post