FEDHA ZA MABADILIKO YA TABIANCHI KUNUFAISHA PANDE MBILI ZA MUUNGANO


Naibu Waziri Wizara Fedha na Mipango Mhe. Hamad Hassan Chande akifunga warsha ya wadau kuhusu upatikanaji wa fedha katika Mifuko mbalimbali ya tabianchi duniani na maandalizi ya Mkutano wa Ishirini na saba wa Nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 27). Warsha hiyo ya siku nne imefanyika katika Hotel ya Kibo Palace, Arusha na kushirikisha Wadau kutoka Serikalini, Mashirika ya Kitaifa, Asasi za Kiraia na taasisi za kifedha

Sehemu ya wadau wa Mazingira wakishiriki katika mjadala kuhusu wigo wa upatikanaji fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kuelekea Mkutano wa Ishirini na saba wa Nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 27). Mjadala huo uliongozwa na Bw. Bakari Machumu Mkurugenzi Mtendaji kutoka Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd.

Naibu Waziri Wizara Fedha na Mipango Mhe. Hamad Hassan Chande akiwa katika picha ya Pamoja na wadau wa mazingira mara baada ya kufunga warsha ya wadau kuhusu upatikanaji wa fedha katika Mifuko mbalimbali ya tabianchi duniani na maandalizi ya Mkutano wa Ishirini na saba wa Nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 27). Kikao hicho cha siku nne kimefanyika katika Hotel ya Kibo Palace, Arusha na kuratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Benki ya Dunia Tawi la Tanzania.

*************************

Naibu Waziri Wizara ya Fedha na Mipango Mhe. Hamad Hassan Chande amesema Mabadiliko ya tabianchi ni halisi na athari zake tayari zinaonekana sio tu katika Mazingira bali pia katika Ukuaji wa uchumi na jamii kwa ujumla.

Naibu Waziri Chande amesema hayo wakati wa kufunga warsha iliyofanyika kwa muda wa siku nne kuanzia 3 - 6 Oktoba 2022 katika hotel ya Kibo Palace, jijini Arusha. Warsha hiyo ilijadili kuhusu upatikanaji wa fedha katika mifuko mbalimbali ya mabadiliko ya tabianchi duniani na maandalizi ya Mkutano wa ishirini na saba wa nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (cop27)

Ametoa rai kwa washiriki hao kuweka nguvu ya pamoja katika kutafuta rasilimali fedha zitakazowezesha kuwa na ufanisi na tija katika jitihada za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika pande zote mbili za Muungano.

“Kwa niaba ya Wizara ya Fedha ninaomba kuahidi kuwa Wizara itandelea kutoa ushirikiano kwa wadau wote ili kuiwezesha nchi yetu kuongeza rasilimali fedha na kuwezesha kunusuru hali za jamii zetu tunazoziongoza” Chande alisitiza

Awali Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt. Omar Shajak amesema katika siku nne za warsha hiyo mijadala mbalimbali juu ya masuala muhimu kama vile kuongeza wigo wa upatikanaji wa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, utekelezaji wa mchango wa Taifa wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022-2032) zilijadiliwa.

Mada nyingine ni Mafanikio na changamoto za Miradi mbalimbali ya kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi, Usimamizi wa biashara ya Kaboni, Mifumo ya dhamana za bluu (Blue Bond Machanism) na Msimamo wa nchi kuelekea Mkutano wa 27 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika 6-11, Novemba 2022 huko Sharm El Sheikh nchini Misri

Warsha hiyo ya siku nne imeandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Benki ya Dunia Tawi la Tanzania na kuhudhuriwa na wajumbe kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Benki ya Dunia nchini, Wanadiplomasia, Wadau wa Maendeleo, Wakurugenzi kutoka Wizara, Idara na Taasisi zake, wawakilishi wa Benki na Taasisi za Fedha, Wawakilishi wa Asasi za Kiraia na Wajumbe kutoka Sekta Binafsi,

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post