NYUKI WAVAMIA MKUTANO WA UCHAGUZI CCM ...WAJUMBE WAJERUHIWA

Katika hali isiyo ya kawaida, jana Oktoba 2, 2022 nyuki walivamia ukumbi wakati uchaguzi ukiendelea wa kumpata Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbeya Vijijini.

Tukio hilo ambalo lilishangaza wengi, lilitokea wakati wa mapumziko wajumbe wakisubiri utaratibu wa kurudia uchaguzi baada ya wagombea kutofikia idadi ya kura stahiki.

Kabla ya kurudiwa uchaguzi, wagombea walikuwa watatu akiwa ni Akimu Mwalupindi, Japhet Mwanasenga na Ramadhan Mwandala ambapo mshindi alipaswa kufikisha nusu ya kura ya wajumbe.

Katika kura za awali kabla ya uchaguzi kurudiwa, Mwalupindi alipata 682, Mwanasenga 500 na Mwandala akipata 218 na msimamizi kuamuru ngoma kurudiwa.

Wakati uchaguzi ukirudiwa hali ilibadilika ukumbini kwa kuzingirwa na nyuki wengi ambao haikufahamika walipotoka na kuwafanya wajumbe wengi kutawanyika na kukimbia bila kupiga kura.

Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa CCM Mkoani Mbeya, Jacob Mwakasole alithibitisha kutokea tukio hilo na kwamba tukio hilo liliwaacha na mshangao kwani wajumbe wawili waliumia na kupelekwa hospitali.

Chanzo: Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post