PURA, KILWA DC WAJADILI MAANDALIZI YA MIONGOZO YA CSR

Kaimu Mkurugezi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Bi. Grace Mwambe (wa pili kulia) na Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wazawa na Uhusishwaji wa Wadau kutoka PURA, Bw. Charles Nyangi (wa pili kushoto) katika mazungumzo yaliyolenga kujadili maandalizi ya miongozo ya Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (Corporate Social Responsibility - CSR). Wengine walioshiriki kikao hicho ni Bw. Ebeneza Mollel kutoka PURA (wa kwanza kulia) na Bw. Kasuka John kutoka Kilwa DC (wa kwanza kushoto)

***************************

MMamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imefanya kikao na Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa (Kilwa District Council) kwa lengo la kujadili maandalizi ya miongozo ya Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (Corporate Social Responsibility - CSR) kwa mujibu wa Kifungu Namba 222 cha Sheria ya Petroli ya mwaka 2015.

Kikao hicho kimefanyika tarehe 28 Agosti, 2022 katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa na kuhudhuriwa na Kaimu Mkurugezi wa Halmashauri hiyo, Bi. Grace Mwambe na Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wazawa na Uhusishwaji wa Wadau kutoka PURA, Bw. Charles Nyangi.

Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Nyangi alieleza kuwa Sheria ya Petroli (2015) imezipa Mamlaka za Serikali za Mitaa/Vijiji jukumu la kuandaa miongozo ya utekelezaji wa CSR ili kuhakikisha kuwa miradi ya CSR inayotekelezwa na kampuni zinazofanya shughuli za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini katika maeneo yao inaendana na mahitaji halisi ya wananchi wa maeneo husika.

“Baadhi ya kampuni zimekuwa zikitekeleza miradi ya CSR kwa kadiri wanavyoona inafaa pasipo kushirikisha jamii husika. Matokeo yake unakuta kwamba kampuni inatekeleza miradi ambayo sio kipaumbele kwa jamii au unakuta jamii hiyo haina uhitaji wa miradi iliyotekelezwa. Kwa kuwa na miongozo ya utekelezaji wa CSR kutawezesha kampuni na jamii kukubaliana miradi ya kutekeleza hivyo kuleta tija kwa pande zote" alieleza Bw. Nyangi.

Kwa upande wake, Bi. Grace aliishukuru PURA kwa kuwafikia na kuwajulisha takwa hilo la kisheria kwa kuwa hawakuwa wanafahamu kuhusu hilo. Aidha, Bi. Grace alieleza kuwa kwa sasa Halmashauri hiyo haina miongozo mahususi ya utekelezaji wa CSR ingawa kuna Hati ya Makubaliano (Memorandum of Understanding – MoU) baina yake na kampuni za mafuta na gesi inayolenga kuhakikisha kuwa wanahusishwa katika kuanisha miradi ya CSR.

Mazungumzo yaliyofanyika yameweka msingi mzuri wa maandalizi ya miongozo hiyo ambayo itakuwa na manufaa kwa pande zote yani jamii na kampuni husika.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post