MASANJA AIPONGEZA KAMATI YA KITAIFA MAANDALIZI YA MKUTANO WA 65 WA SHIRIKA LA UTALII DUNIANI


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) ameipongeza Kamati ya Kitaifa ya Maandalizi ya Mkutano wa 65 wa Shirika la Utalii Duniani-Kamisheni ya Afrika(UNWTO) kwa kuendelea na maandalizi mazuri ili kufanikisha mkutano huo unaotarajiwa kufanyika Oktoba 5-7, 2022 katika ukumbi wa mikutano wa Gran Melia jijini Arusha.

Ameyasema hayo leo katika kikao cha tatu cha Kamati hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa jijini Arusha.

Mhe. Masanja amewataka wanakamati hao kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha mkutano wa UNWTO unafanikiwa kwa kiwango cha juu.

“Ninaamini timu hii ni timu iliyokamilika hivyo kila mjumbe atumie uwezo wake kufanya kazi vizuri ili tusimuangushe Mheshimiwa Rais” Mhe.Masanja amesisitiza.

Ameongeza kuwa lengo la mkutano wa UNWTO ni kuitangaza Tanzania itakayosaidia kuongeza idadi ya watalii na wawekezaji nchini.

Naye, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii,Juma Mkomi amesema Wizara itatoa ushirikiano wa kutosha katika kufanikisha mkutano huo na pia kutatua changamoto zitakazojitokeza.

Mkutano huo utahudhuriwa na Katibu Mkuu wa Shirika la Utalii Duniani (UNWTO), Zurab Pololikashvili, Mawaziri na viongozi wenye dhamana ya kusimamia masuala ya utalii kutoka Nchi Wanachama wa Shirika la Utalii Duniani Kamisheni ya Afrika.

Kauli mbiu ya mkutano huo ni “Kuujenga Upya Utalii Stahimilivu wa Afrika kwa Maendeleo Jumuishi ya Kiuchumi na Kijamii”.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post