TAASISI YA ITF KUKABILIANA NA CHANGAMOTO YA WANAWAKE WENYE ULEMAVU KUJIFUNGUA KATIKA MAZINGIRA MAGUMU

Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, iliyopo Dodoma, Dk. Alphonce Chandika, (kulia) akipokea msaada wa kitanda maalum cha cha kujifungulia Wanawake walemavu kutoka kwa mwasisi wa taasisi ya Ikupa Trust Foundation na Mbunge wa viti maalum Mh. Stella Ikupa (katikati) na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Bw. Amon Mpanju, katika hafla iliyofanyika jijini Dodoma . Msaada huu umetokana na sehemu ya fedha zilizotolewa taasisi ya Nos Vies en Partage Foundation (NVeP) ,inayofadhiliwa na Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Barrick Gold Corporation, Mark Bristow. Wengine pichani ni Wafanyakazi wa hospitali hiyo.
Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, iliyopo Dodoma, Dk. Alphonce Chandika, (kulia) akipokea msaada wa kitanda maalum cha cha kujifungulia Wanawake walemavu kutoka kwa mwasisi wa taasisi ya Ikupa Trust Foundation na Mbunge wa viti maalum Mh. Stella Ikupa (katikati) na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Bw. Amon Mpanju, katika hafla iliyofanyika jijini Dodoma.
Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Bristow, akikabidhi vocha ya Dola za kimarekani 10,000 kwa Meneja Miradi wa taasisi ya Ikupa Trust Fund, Peter Charles, kwa ajili ya kusaidia miradi ya akina mama na watoto wenye ulemavu alipofanya ziara ya kikazi nchini karibuni.
***

Taasisi ya Ikupa Trust Foundation (ITF) ambayo mwasisi wake ni Mbunge wa viti Maalum, Mh. Stella Ikupa, imekabidhi msaada wa kitanda maalum cha kujifungulia Wanawake walemavu, chenye thamani ya shilingi milioni moja na laki tatu kwa hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma.


Msaada huu umetokana na sehemu ya fedha zilizotolewa taasisi ya Nos Vies en Partage Foundation (NVeP), inayofadhiliwa na Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Barrick Gold Corporation, Mark Bristow. Akiwa nchini hivi karibuni, Bw Bristow alikabidhi msaada wa dola 10,000 kwa taasisi ya hiyo kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za Wanawake wenye ulemavu.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi kitanda hicho , Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Bw. Amon Mpanju, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Ikupa Trust Foundation, taasisi ambayo inashughulika na masuala ya watu wenye ulemavu amesema wametoa msaada huo ikiwa ni moja ya jitihada za kuwarahisishia upataji huduma Wanawake wenye ulemavu.

“Sisi kama Ikupa Trust Foundation, tumeona tuanze kwa mfano kuja hapa katika hospitali hii ya Benjamin William Mkapa kukabidhi hiki kitanda lakini msaada huu tutaenda kutoa pia katika Mkoa wa Shinyanga na Dar es salam kwa kuanzia na mipango tiliyonayo ifikapo mwezi Juni 2023 tuwe tumekabidhi vitanda vipatavyo hamsini katika hospitali mbalimbali hapa nchini", Alisema Bw. Amon Mpanju.

Mwasisi wa taasisi hiyo na Mbunge wa Viti Maalumu kundi la wenye ulemavu, Stella Ikupa, amesema anaishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kujali sana kundi la watu wenye ulemavu kwa kuona umuhimu wa kuwa na vyumba Maalum vya kujifungulia wanawake wenye ulemavu na kuelekeza watendaji wa Serikali yake kulifanyia kazi suala hili.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Benjamin William Mkapa Dkt Alphonce Chandika, aliishukuru Taasisi ya Ikupa kwa kuwapatia kitanda hicho kwa kuwa kitafanikisha kuongeza ufanisi katika kuhudumia akina mama wajawazito wenye ulemavu.

Dkt. chandika, aliongeza kusema kuwa Hospitali ya Benjamin Mkapa, inawajali Wanawake wenye ulemavu, hivyo wasisite kufika na kupata huduma kwani watafurahia kwa sababu wameshatenga chumba maalumu kwa ajili yao kwa ajili ya kuhakikisha kunakuwa na staha ya kuhusumiwa katika mazingira rafiki.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post