AFARIKI KWA KUUNGUA MOTO CHUMBANI KWAKE SHINYANGA MJINI


Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Mwanaume mmoja mkazi wa mtaa wa Luhende kata ya Masekelo Manispaa ya Shinyanga, Ngelela Seleli mwenye umri wa miaka 40 amefariki dunia kwa kuungua moto akiwa ndani ya chumba chake cha kulala.

Misalaba Blog imefika kwenye eneo la tukio na kuzungumza na Mwenyekiti wa mtaa wa Luhende Msafiri Nadula ambaye amesema tukio hilo limetokea leo Septemba 7,2022 majira ya saa nane usiku na kwamba mwenyekiti Nadula amesema amepata taarifa hizo kutoka kwa wananchi wa mtaa huo.


Nadula ameeleza kuwa marehemu Ngelela Seleli alikuwa na ugonjwa wa kifafa ambapo pia alikuwa ni mjasiriamali mdogo akijishughulisha na biashara ya kuuza vifaa mbalimbali ikiwemo vyuma chakavu.


“Mimi nimefika kwenye tukio nikakuta wananchi wanajitihada za kuuzima moto lakini tulipoangalia alimokuwa amelala alikuwa tayari ameungua kabisa mwili wote ikabidi nipige simu polisi ndiyo wamekuja kuuchukua mwili”,amesema.

“Lakini pia marehemu alikuwa na ugonjwa wa akili japo alikuwa anajitambua na alikuwa anafanya biashara yake vizuri na kodi alikuwa analipa mwenyewe”, amesema Nadula.

Wakizungumza baadhi ya wananchi walioshuhudia tukio hilo wameeleza namna walivyoguswa na msiba wa marehemu Ngelela Seleli ambaye alikuwa ni mpangaji katika nyumba ya Khadija Issa maarufu kwa jina la Mama Said.


Misalaba Blog pia imefika katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga na kuzungumza na mganga mfawidhi Dkt. Luzila John ambaye amekiri kuupokea mwili wa marehemu huyo majira ya saa kumi na moja asubuhi.

“Mnamo saa kumi na moja alfajiri tulipokea mwili wa marehemu ambaye alikuwa amesadikika kuungua moto anaitwa Ngelela Seleli wa kiume ambaye sisi tulimpokea akiwa tayari ameshafariki kwa hiyo tulithibitisha kifo”, amesema Dkt. Luzila.


Kwa upande wake Kamanda wa jeshi la polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna wa polisi Janeth Magomi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akisema jeshi hilo linaendelea na jitihada za kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha tukio.

CHANZO - MISALABA BLOG


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post