KAMATI YA BUNGE YAITAKA OSHA KUONGEZA ELIMU KWA UMMA


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Hesabu za Serikali (PAC), Mhe. Naghenjwa Kaboyoka (kushoto) akizungumza na Wajumbe wa Kamati hiyo pamoja na Viongozi wa OSHA wakati mafunzo ya usalama na afya yaliyotolewa na OSHA kwa Kamati hiyo ambayo yalienda sambamba na zoezi la ukaguzi wa jengo jipya la Ofisi za OSHA jijini Dodoma. Aliokaa nao meza kuu ni Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi ya OSHA, Dkt. Adelhelm Meru na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi Khadija Mwenda.


Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi Khadija Mwenda (kulia) akitoa maelezo ya awali kuhusu Taasisi ya OSHA mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Hesabu za Serikali (PAC) wakati wa ziara ya Wajumbe wa Kamati hiyo katika Ofisi za OSHA jijini Dodoma iliyolenga kujifunza kuhusu masuala mbalimbali ya usalama na afya mahali pa kazi. Waliokaa katika meza kuu ni Mwenyekiti wa Bodi ya OSHA, Dkt. Adelhelm Meru (wapili kulia), Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Mhe. Naghenjwa Kaboyoka na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Japhet Hasunga.


Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi ya OSHA, Dkt.Adelhelm Meru (aliyesimama) akitoa neno la ukaribisho kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Hesabu za Serikali (PAC) wakati wa kikao kifupi mara baada ya Wajumbe hao kufika katika Ofisi za OSHA jijini Dodoma.


Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Hesabu za Serikali (PAC) wakifuatilia mada mbali mbali zilizowasilishwa na watalaam wa OSHA wakati mafunzo na zoezi la upimaji afya kwa Wajumbe wa Kamati hiyo katika Ofisi za OSHA Jijini Dodoma.


Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Hesabu za Serikali (PAC) wakishiriki zoezi la uchunguzi wa afya lililoendeshwa na wakaguzi wa afya wa OSHA kwa Wajumbe hao katika Ofisi za OSHA Jijini Dodoma.


Mbunge wa Viti Maalam wa Mkoa wa Morogoro na Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Hesabu za Serikali (PAC) Mhe. Aleksia Kamguna (aliyesimama), akichangia mada wakati wa majadiliano kati ya OSHA na Kamati hiyo kuhusu masuala mbalimbali ya usalama na afya mahali pa kazi.


Mbunge wa Jimbo la Katavi na Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Hesabu za Serikali (PAC) Mhe. Isack Kamwelwe, akifanyiwa kipimo cha usikivu (audiometry test) na Mkaguzi wa Afya wa OSHA, Dkt. Kihama Kilele. Zoezi hilo lilifanyika kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali sambamba na mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi.

**************************

Na Mwandishi Wetu

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeutaka Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kuongeza uelewa wa masuala ya usalama na afya miongoni mwa Watanzania ili kupunguza ajali, magonjwa na vifo vinavyotokea kwenye maeneo ya kazi.

Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Naghenjwa Kaboyoka, alipozungumza baada ya kuhitimishwa kwa mafunzo ya usalama na afya pamoja na zoezi la upimaji afya lililoandaliwa na OSHA kwa Kamati hiyo.

“Wajumbe wangu kwakweli wamefurahi sana maana wamejua mambo mengi sana kupitia mada nzuri zilizowasilishwa na watalaam wa OSHA. Tathmini ambayo tunatoka nayo baada ya mafunzo haya ni kwamba OSHA inafanya kazi nzuri lakini tunawashauri kujitangaza na kutoa elimu zaidi kwa wananchi ili kuwasaidia waajiri na wafanyakazi kujua wajibu wao kuhusiana na usalama na afya mahali pa kazi,” ameeleza Naghenjwa Kaboyoka, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali.

Mafunzo hayo yaliyofanyika leo (Septemba 03, 2022) katika jengo jipya la OSHA la Dodoma, yalilenga kuwajengea uelewa wa masuala ya usalama na afya wabunge hao ikiwa ni mkakati wa Taasisi wa kuyafikia makundi mbali mbali katika jamii.

Aidha, pamoja na kupatiwa mafunzo hayo muhimu, watunga sera hao walikuwa na lengo la kukagua jengo jipya la OSHA ili kujiridhisha endapo ujenzi huo umezingatia viwango stahiki ambapo wameleza kuridhishwa na kiwango cha jengo hilo pamoja na kiasi cha fedha za umma zilizotumika.

Awali, menejimenti ya OSHA iliwasilisha mada mbali mbali mbele ya Kamati hiyo ikiwemo namna ilivyotekeleza mradi huo wa jengo la ofisi la ghorofa nne kwa muda wa miezi nane (8) na kutumia kiasi cha bilioni 4.8 chini ya bajeti ya bilioni 6.5 pamoja na kodi.

Wakizungumza mara baada ya kuhitimisha mafunzo, baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo wameipongeza OSHA kwa kusimamia vyema mradi huo na kuokoa fedha nyingi za serikali ambapo wamezitaka Taasisi nyingine za serikali kuiga mfano wa OSHA.

“Tumepata mafunzo mazuri sana, kule nje wengine tulikuwa tunasikia tu OSHA bila kujua namna wanavyofanya kazi lakini leo tumejifunza kwamba OSHA wanafanya kazi kwa kuzingatia taratibu zote walizoelekezwa kisheria.

Aidha, jambo kubwa lililotufurahisha zaidi ni kuhusu ujenzi wa jengo hili. Kiuhalisia mimi kama mjumbe wa kamati ya PAC nimeona thamani halisi ya fedha katika jengo (value for money). Jengo limejengwa vizuri na limezingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu na taratibu zote za usalama na afya. Tunatoa wito kwa Taasisi nyingine kuiga mfano huu,” amesema Emmanuel Shangai, Mjumbe wa Kamati na Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro.



Kwa upande wao Mwenyekiti wa Bodi ya OSHA, Dkt. Adelhelm Meru na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, wameeleza dhumuni la kuandaa mafunzo hayo na kuahidi kutekeleza ushauri uliotolewa na Kamati hiyo yenye wajibu wa kusimamia nidhamu katika matumizi ya fedha za serikali.

Kwetu OSHA, imekuwa siku nzuri sana ambapo tumepata fursa ya kukutana na wajumbe wa Kamati hii. Kama tunavyofahamu wabunge ni wawakilishi wa wananchi ambao ni wadau wetu hivyo kukutana nao na kujadiliana kuhusu masuala haya muhimu kutawezesha wadau wetu kupata elimu ya masuala haya kupitia wabunge katika majimbo yao,” amesema Dkt. Adelhelm Meru, Mwenyekiti Bodi ya OSHA.

“Sisi kama watendaji tumefarijika sana kupata fursa ya kuwashirikisha waheshimiwa wabunge masuala haya ya usalama na afya mahali pa kazi kwani wao ndio wanaotunga sera na kuishauri serikali hivyo wakiyafahamu vema majukumu yetu ndivyo watakavyoweza kuishauri vizuri serikali,” amesema Bi. Khadija Mwenda, Mtendaji Mkuu wa OSHA.

Ziara hiyo imefanyika sambamba na mafunzo ya Usalama na Afya kwa wajumbe wa Kamati hiyo pamoja na zoezi la uchunguzi wa afya zao ili kuwawezesha kufahamu kwa undani shughuli zinazofanyika na Taasisi ya OSHA na hivyo kuwa mabalozi kwa wananchi wanaowawakilisha.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post