WAZIRI NAPE AIPONGEZA KAMATI YA MAUDHUI YA TCRA


KAMATI ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imemwagiwan pongezi nyingi kwa kazi nzuri ya kulinda maadili ya jamii kwa kuhakikisha Vyombo vya Utangazaji pamoja na Mitandao ya Kijamii inazingatia miiko ya Uandishi na Utangazaji wa Habari nchini.

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alitoa pongezi hizo jana (Jumapili) alipokuwa akiongea na Waandishi wa Habari katika ofisi za Makao Makuu ya TCRA, jijini Dar es Salaam.

"Ninawapongeza Kamati ya Maudhui ya TCRA kwa kazi nzuri sana ya kulinda maadili ya jamii yetu," alisema Waziri huyo.

Waziri Nape aliihakikishia jamii kuwa maudhui yanayotolewa na vyombo vya Utangazaji vilivyosajiliwa nchini ni salama.

Alisema TCRA inaendelea kufanya kazi nzuri kwa kuhakikisha kuwa anga la Tanzania linabakia salama na maudhui ya Vyombo Vya Utangazaji hayaiharibu jamii kwa maudhui yasiyofaa.

Alitoa onyo kali kwa wale wote watakaopatikana wakisambaza maudhui ya ushoga na usagaji kupitia mitandao yA kijamii na kuzua taharuki kwa wananchi na kuahidi hatua kali kuchukuliwa kwa wakosaji.

Aliwataka ma Admin wa WhatsApp na wamiliki wa Televisheni za viganjani (Online TV) kuhakikisha maudhui hasi yanafutwa na hayasambazwi vinginevyo hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watakaokaidi.

Katika Mkutano huo na Waandishi wa Habari, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabiri BAkari pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Maudhui, Jacob Tesha na Derek Murusuri, walihudhuria.

Kamati ya Maudhui ya TCRA ina jukumu la kusimamia na kufuatilia maudhui yote yanayorushwa katika Vyombo vya Utangazaji na Mitandao ya Kijamii iliyosajiriwa nchini.

Kamati hiyo inayoundwa na Waziri mwenye dhamana ya Habari, vilevile ina jukumu la kusumamia maadili ya Utangazaji pamoja na kumshauri Waziri wa sekta kuhusu masuala ya kisera.

Tanzania imekuwa mojawapo ya nchi kiongozi katika masuala ya "cyber ecosystem" katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na pia katika mataifa ya SADC.

Wakati huo huo, Rais Samia Suluhu Hassan pia amepigilia msumari hitaji la wazazi kusimamia maadili ya watoto na wasiiachie teknolojia ya mitandao ya kijamii kuwalelea watoto wao.

Rais aliyasema hayo jana katika hafla ya kuadhimisha jubilee ya miaka 50 ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana.

Rais aliwataka wazazi wawaelimishe watoto wao matumizi sahihi ya teknolojia ya mawasiliano ili wasitumie mitandao watakavyo.
CHANZO-EATV





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post