Waziri wa Ujenzi , Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Dk. Khalid Salum Mohamed akizungumza na Menejimenti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wakati Waziri huyo alipotembelea Mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Masuala ya Kisekta wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dk.Emmanuel Manase akizungumza hali ya mawasiliano na Jiographia Zanzibar katika Mawasiliano walivyoweza kutoa wakati ziara ya Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Dk.Khalid Salum Mohamed alipotembelea Mamlaka hiyo Jijini Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Dk.Jabir Bakari akizungumza kuhusiana na mikakati ya TCRA katika kutoa huduma bora kwa pande zote kwa Tanzania Bara na Zanzibar kwenye sekta ya mawasiliano kwenye kikao kazi cha Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Dk.Khalid Salum Mohamed wakati alipotembelea Mamlaka hiyo Jijini Dar es Salaam.
****************************
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dk Khalid Salum Mohamed amesema kuwa katika kwenda na mabadiliko ya Teknolojia ni kazi kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ni kuwekeza kuwaongezea utaalamu wa viwango vya kimataifa wafanyakazi katika kudhibiti makosa ya usalama mtandaoni.
Akizungumza wakati alipotembelea mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam, Dk Mohamed amesema teknolojia imekuwa ikibadilika kwa kasi na kusababisha changamoto nyingi zinazoikabili sekta ya mawasiliano ikiwemo makosa ya usalama mtandaoni wa watumiaji wa mwisho.
Amesema ili kudhibiti makosa hayo, ni lazima TCRA kuwekeza kwenye kuwapatia mafunzo ya kitaalamu yanayokubalika kimataifa katika kudhibiti makosa hayo na kupunguza hasara katika nchi kwani teknolojia ina faida na hasara
"Ni muhimu jamii kuelimishwa zaidi kuhusu majanga ya kimtandao ambayo yamekuwa yakihatarisha usalama wa nchi na mifumo ya mawasiliano Tanzania Bara ikiharibika, maana yake mawasiliano ya Jamuhuri ya Muungano yameharibiwa na kujenga kwake ni gharama inayotokana na watalaam kupewa mafunzi yasiyotarajiwa" amesema Dk Mohamed.
Pia alieleza kuwa mamlaka hiyo inatarajia kuingia mkataba wa makubaliano na Shirika la Viwango Zanzibar (ZBS) kwa ajili ya ukaguzi wa vifaa vya mawasiliano vinavyoingia kutoka nje ya nchi katika kudhibiti bidhaa za mawasiliano.
Aliongeza kuwa TCRA kwa kushirikiana na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) zimejenga minara 42 ya mawasiliano katika visiwa vyote 42 hivyo imesaidia kuondoa changamoto ya mawasiliano kwa wakazi wa maeneo hayo.
"Muendelee kushirikiana katika kuboresha ustawi wa sekta ya mawasiliano kwa sababu ni ya muungano hivyo rasilimali zilizopo zitumike kustawisha jamii kwa kujenga uchumi imara na kuleta maendeleo. Pia mnapaswa kuona namna ya kutekeleza sera ya uchumi wa buluu katika kuhakikisha wananchi wote wanapata mawasiliano bora," alisisitiza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TCRA, Dk Jabir Bakari alisema kuwa wataendelea kuhakikisha wanatoa ushauri wa kitaalamu kwa kampuni za simu ili kutoa huduma bora za mawasiliano.
Pia amesema kuwa yapo maeneo mawili ya muungano ambayo mamlaka hiyo huyashughulikia ikiwemo mawasiliano na posta ambayo yanatakiwa kutoa matokeo chanya katika uchumi wa buluu na uchumi wa kidigitali.
"Tutafanyia kazi maelekezo tuliyopewa ya kuhakikisha Zanzibar inakuwa na huduma bora za mawasiliano katika visiwa vyote vidogovidogo," alisema Dk Bakari.