MAABARA MPYA YA UPIMAJI SAMPULI ZA UVIKO-19 TANGA, KURAHISISHA UPATIKANAJI WA HUDUMA KWA HARAKA


Na Mwandishi Wetu, Tanga.

Maabara mpya ya upimaji wa sampuli za UVIKO-19 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bombo, Tanga itarahisisha upatikanaji wa huduma kwa haraka zaidi hivyo kuwapunguzia wananchi adha ya kusubiri majibu kwa muda mrefu.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Afya Mhe Ummy Mwalimu kwenye hafla fupi ya uzinduzi wa Maabara ya upimaji wa sampuli za UVIKO-19 iliyofanyika Agosti 15, 2022 katika Hospitali ya Rufaa Bombo, Tanga iliyohudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Maendeleo na Ushirikiano wa Uchumi kutoka Serikali ya Ujerumani Dkt. Bärbel Kofler.

"Tumefungua kituo hiki cha kupima sampuli za UVIKO-19 kwa kutumia kipimo hiki cha PCR , sasa hivi kikianza kufanya kazi hapa Bombo mtu akipima UVIKO-19 majibu yanaweza kutoka mapema ndani ya masaa nane " amesema Waziri Ummy.

Amesema kuwa hapo awali sampuli za vipimo za UVIKO-19 zilikuwa zinatumwa kwenda Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii Jijini Dar Es Salaam hivyo kuchukua muda mrefu kwa wananchi kusubiri majibu.

Waziri Ummy amesema kuwa ujenzi wa maabara hiyo umegharimu kiasi cha Shilingi Milioni 225 huku ikiwa ni maabara ya 11 nchini yenye uwezo wa kufanya vipimo hivyo vya UVIKO-19.

Aidha Waziri Ummy ameishukuru Serikali ya Ujerumani kwa kuendelea kusaidia Sekta ya Afya nchini kupitia Programu ya Tumaini la Mama ambayo imelenga kuboreshaji wa utoaji wa huduma bora za afya kwa kutoa Bima za Afya kwa Mama wajawazito na watoto wao (wasio na uwezo)

Kwa Upande wake Dkt. Bärbel Kofler Naibu Waziri wa Maendeleo na Ushirikiano wa Uchumi nchini Ujerumani amesema kuwa wanaamini kituo hicho sasa kinakwenda kutoa huduma za vipimo kwa wakazi wa Tanga na maeneo jirani ya hapa. Kuna umuhimu mkubwa sana kwetu sisi Ujerumani kushirikiana na mataifa mengine katika mapambano dhidi ya UVIKO-19.

Dkt. Kofler amesema kuwa Serikali ya Ujerumani inaendelea na mpango wa kusaidia nchi nyinginezo ulimwenguni kupata chanjo dhidi ya UVIKO-19 na wamejipanga kutoa dozi zaidi ya Bilioni 7.2 za chanjo dhidi ya UVIKO-19

Aidha Dkt. Kofler ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutoa hamasa na elimu ya chanjo dhidi ya UVIKO-19 na kuahidi kuwa Serikali ya Ujerumani itaendelea kushirikiana na Tanzania katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo pamoja na mambo mengine

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments