WAUGUZI WALALAMIKIA MUUNDO WA AFYA KWENYE HALMASHAURI


Rais wa Chama cha wauguzi Tanzania (TANNA), Alexander Baluhya (kulia) akizungumza na waandishi wa habari mjini akiitaka serikali kutotekeleza maboresho ya muundo wa vitendo vya idara ya sekta ya afya kwenye halmashauri na ngazi za mikoa .(Picha na Fadhili Abdallah)
Rais wa Chama cha wauguzi Tanzania (TANNA), Alexander Baluhya (wa pili kulia) akizungumza na waandishi wa habari mjini akiitaka serikali kutotekeleza maboresho ya muundo wa vitendo vya idara ya sekta ya afya kwenye halmashauri na ngazi za mikoa

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

 

WAUGUZI nchini wameiomba serikali kuangalia upya muundo wa utawala katika mamlaka za serikali za mitaa ambao unaiondoa kada ya uuguzi kuwa na kiongozi wke ambaye anaweza kusimamia na kuzungumzia changamoto zinazowakabili.

 

Rais wa Chama cha wauguzi Tanzania (TANNA), Alexander Baluhya  akizungumza na waandishi wa habari mjini Kigoma alisema kuwa kwa sasa hakuna kiongozi anayesimama kwa niaba ya wauguzi kwenye mamlaka za serrikali za mitaa badala yake uwakilishi wao unabaki kwa Mganga Mkuu wa wilaya.

 

Raisi huyo wa  TANNA alisema kuwa hawakubaliani na muundo mpya wa utawala wa mamlaka za serikali za mitaa Tanzania wa mwaka 2022 ambao hautoi mazingira mazuri ya uwakilishi wao kwenye mamlaka za maamuzi na hasa ukizingatia kwa sasa idadi kubwa ya watumishi kwenye mamlaka hiyo ni wauguzi wakifuatilia kwa kada ya ualimu.

 

“ Ni vema serikali ikaufanyia maboresho muundo huu ili kutoathiri huduma za afya nchini hususani kwenye ngazi za halmashauri  na mikoa kwani kada nzima ya uuguzi ni vizuri kuwa na kitengo kinachojitegemea ili changamoto na maslahi yao yaweze kushughulikiwa kwa haraka kuliko ilivyo hivi sasa,”alisema Baluhya.

 

Alisema wauguzi na wakunga katika sekta ya afya hapa nchini ni zaidi ya asilimia 60, na asilimia 80 ya kazi zote za idara ya afya hutolewa nao moja kwa moja kwa wagonjwa na wateja.

 

Kwa upande wake Katibu msaidizi wa TANNA mkoa wa Kigoma, Bertha Anderson alisema ni vizuri serikali ikaliangalia upya suala la muundo huo ili kuifanya kada hiyo iweze kujisimamia na kujisemea kulingana na changamoto zinazowakabili .

 

Katibu huyo Msaidizi alisema kuwa ni vizuri kwa sasa wauguzi wakaungana pamoja kupigania jambo hilo ili serikali iweze kulitekeleza kwani suala hilo ni la kitaaluma na wao kama wana taaluma wanapaswa kusimamia pamoja kupigania haki yao.

 

Afisa Muuguzi Msaidizi kutoka hospitali ya rufaa ya mkoa Kigoma Maweni, Marry Stella alisema serikali imeweza kuwongeza wauguzi kwenye hospitali hiyo jambo ambalo limesaidia kuerahisisha utendaji kazi kwa kupeana zamu ukilinganisha na mzigo mkubwa wa utendaji waliokuwa nao awali.

 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post