DIAMOND PLATNUMZ AVUNJA REKODI AKIAMSHA AMSHA KAMPENI ZA UCHAGUZI KENYA


Raila Odinga mgombea urais nchini Kenya akiwa na Supastaa wa Afrika kutoka Tanzania Diamond Platnumz
Diamond Platnumz akitumbuiza nchini Kenya

DIAMOND PLATNUMZ; ni staa mkubwa wa muziki barani Afrika ambaye ameweka rekodi nyingine ya kulipwa pesa nyingi za shoo ndani ya muda mfupi.


Jumamosi iliyopita ya Agosti 6, 2022 Diamond au Mondi alikuwa mmoja wa watumbuizaji katika hafla ya Mgombea Urais wa Kenya, Raila Odinga katika Uwanja wa Kasarani nchini humo.


Jumatano iliyopita Diamond alitangaza ratiba yake na kusema kwamba Jumamosi angetumbuiza nchini Kenya kabla ya kujiandaa kwenye matamasha mengine makubwa mwishoni mwa mwezi huu nchini Canada.


Sasa; vyanzo vya habari nchini humo vinasema kuwa, baada ya kupiga shoo ya kihistoria, Diamond alilipwa na timu ya kampeni ya Raila kiasi cha shilingi milioni 10 za Kenya ambazo ni takriban shilingi milioni 200 za Kitanzania.


Diamond ambaye alikuwa nchini Afrika Kusini kwa ajili ya birthday ya binti yake, Tiffah Dangote alikodisha ndege binafsi akiambatana na binti yake huyo ambapo alikwenda kwenye shoo hiyo ambayo aliifanya kwa dakika 30 tu kisha akavuta kiasi hicho cha pesa.

Baada ya shoo hiyo, Diamond alichukua tena ndege binafsi ambayo ilimrejesha yeye na Tiffah nchini Afrika Kusini kuendelea na pati ambayo ilikuwa ni kufuru tupu.


Diamond alitumbuiza Nairobi mara ya mwisho mnamo Desemba 2018 wakati wa Tamasha la Wasafi Festival kuadhimisha sherehe za Mwaka Mpya ambapo ilikuwa imepita miaka mine bila kufanya shoo Nairobi hivyo shoo hiyo ya Jumamosi ilifurika nyomi ya ajabu kwa kuwa pia ilikuwa ya bure.


Mikutano ya kisiasa nchini Kenya ilifikia kikomo Jumamosi iliyopita kwa mujibu wa agizo la Katiba linalotaka kampeni kukamilika angalau siku mbili kabla ya kuandaliwa kwa uchaguzi mkuu.

Raila Odinga na Diamond Platnumz

Uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika Agosti 9, 2022 (kesho) na kinyang’anyiro hicho kimetajwa kuwa chenye ushindani mkali kuwahi kutokea nchini tangu uhuru.


Wagombea wakuu wa Urais ni kinara wa Azimio la Umoja ambaye ni mwanasiasa wa muda mrefu, Raila Odinga ambaye anajaribu kurusha karata kwa mara ya tano huku mpinzani wake mkubwa akiwa ni naibu wa sasa anayepeperusha bendera ya mrengo wa Kenya Kwanza, William Ruto.

Cc; @sifaelpaul

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post