Tamasha kubwa la Nyama Choma maarufu 'SHY TOWN NYAMA CHOMA FESTIVAL' ambalo hufanyika kila mwaka likikutanisha mabingwa na watalaamu wa kuchoma nyama aina mbalimbali linatarajiwa kufanyika Agosti 26 hadi 28,2022 katika viwanja vya Mazingira Center Mjini Shinyanga.
Akizungumza na Malunde 1 blog kuhusu Tamasha la Shy Town Nyama Choma Festival, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Maandalizi Bi. Annet Lazaro amesema tamasha hilo linatarajiwa kuhudhuriwa na watu zaidi ya elfu 10 huku wachoma nyama maarufu 'mabingwa na wataalamu wa kuchoma nyama' kutoka mikoa na majiji mbalimbali wakioneshana uwezo katika uchomaji nyama kama vile nyama ya ng’ombe, mbuzi, kuku, bata, samaki na soseji n.k.
Annet ameitaja mikoa itakayoshiriki kuwa ni Arusha, Dar es salaam, (Kilimanjaro 'Moshi'), Manyara, Mwanza, Dodoma na Shinyanga.
“Hii ni fursa kubwa kwa taasisi, wafanyabiashara na wadau mbalimbali kama vile Benki, Mashirika ya bima, huduma za viwanda,mabucha,bodaboda,hoteli, madereva tac, bajaji, maduka yote na wanaotoa huduma za kijamii kutangaza huduma zao siku ya Tamasha la Nyama Choma”,amesema Annet.
“Tangu tamasha hili pendwa lianzishwe, limekuwa na mafanikio makubwa na mwaka huu tumejipanga zaidi, tunategemea kufunga zaidi ya tenti 40 ambazo zitatoa huduma mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara,mashirika na taasisi na wadau mbalimbali watakaoshiriki kutoa huduma mbalimbali zikiwemo huduma za chakula na vinywaji”,ameongeza.
Amesema Tamasha hilo litaambatana na michezo mbalimbali ya watoto na burudani kutoka kwa wasanii wa kizazi kipya (Bongo Fleva), Bendi na ngoma za asili, uchangiaji wa damu salama na elimu ya ujasiriamali.
Miongoni mwa wadau wakiwemo wafanyabiashara wa nyama wamesema Tamasha hilo la Nyama Choma ni fursa kubwa kwa wafanyabiashara na watoa huduma za kijamii kutumia tamasha kujipatia kipato zaidi kwani limekuwa na mvuto sana tangu lianzishwe.