RAIS SAMIA : VIJANA NJOONI KWENYE SEKTA YA KILIMO


Rais Samia Suluhu akihutubia kwenye maadhimisho ya Nanenane jijini Mbeya

**
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu amewataka vijana kuchangamkia fursa ya kilimo akieleza kuwa Serikali imejipanga kuwapatia mashamba, kuwapa mikopo kupitia Benki na imetafuta masoko kwa kila zao linalozalishwa.


Rais Samia ameyasema hayo leo Agosti 8,2022 wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wakulima ‘Nane Nane’ ambayo kitaifa imefanyika mkoani Mbeya.


“Vijana njooni kwenye kilimo, vijana ingieni kwenye sekta ya kilimo. Serikali tumejipanga kuwapatia mashamba, tumejipanga kwenye Mabenki kuwapa mikopo nafuu na pia tumejipanga vyema na masoko, kila kinachozalishwa kina soko”,amesema Rais Samia.


Aidha ametoa wito kwa wakulima kuzalisha kibiashabara huku akibainisha kuwa Fedha zinazotolewa na serikali zikasaidie wananchi.

“Serikali imetoa ruzuku kwa wakulima…Wito wangu kwa wakulima Nendeni mlime kibiashara. Usajili wa wakulima, niombe wakulima wote muende mkajisajili, mbele huko tutatoa vitambulisho kwa wakulima, kitambulisho chako hicho ndicho kitakachokufanya uende kupata huduma kadhaa, ikiwa ni mkopo, ruzuku, ikiwa ni mambo mengine, sasa ukifanya uvivu kutokwenda kujisajili, utakapokwenda kutaka huduma huna kitambulisho...hasara itakuwa kwako", amesema Rais Samia.


Aidha Rais Samia ameziagiza Wizara ya Kilimo na Wizara ya Fedha, kuhakikisha fedha za ruzuku ya mbolea ambazo zimeidhinishwa na serikali kwa lengo la kushusha bei ya mbolea nchini, zinaanza kutumika kuanzia tarehe 15 mwezi huu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post