RAIS SAMIA ALETA MAFURIKO YA WATALII

* Zitto atabiri utalii kuingiza dola bilioni 3 kwa mwaka, sawa na Shilingi trilioni 7

* Royal Tour yaleta kishindo

* Watalii wafurika kila kona, ikiwemo Arusha, Zanzibar, Serengeti


IDADI ya watalii wanaokuja nchini baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuongoza ziara ya uzinduzi wa filamu ya Royal Tour nchini Marekani imezidi kuongezeka, huku viwanja vya ndege, mahoteli na mbuga za wanyama zikiona mafuriko ya watalii ambayo hawajawahi kutokea nchini.


Mkoa wa Arusha sasa hivi umetapakaa watalii kutoka nje, kiasi kwamba hata kampuni za watalii zimekumbwa na uhaba wa magari ya kuwapeleka watalii mbugani.


Visiwa vya Zanzibar kwa sasa navyo vinapokea idadi kubwa ya watalii.

"Arusha imejaa watalii" Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, alisema kupitia ukurasa wake wa Twitter Julai 24.

Akimjibu Zitto, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC), Arafat Haji, alisema kuwa Zanzibar nayo inapata mafuriko ya watalii.

Zitto na Haji wote wamezishauri serikali za Tanzania na Zanzibar kuwekeza kwenye upanuzi wa miundombinu, ikiwemo viwanja vya ndege na bandari, ili kukabiliana na ongezeko hilo la watalii.


Zitto amebashiri kuwa huenda Tanzania sasa ikaweka rekodi kwa kupata dola za Marekani bilioni 3 kwa mwaka 2022 kutoka kwenye utalii, sawa na Shilingi trilioni 7.


Mwaka jana, Tanzania ilipata dola za Marekani bilioni 1.4 kutoka kwenye sekta utalii 


Naye Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema kuwa ndege ya Shirika la Ndege la KLM la Uholanzi usiku wa tarege 1 Agosti mwaka huu imeshusha abiria zaidi ya 250 katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).


"Kwa kweli kishindo ambacho Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Samia amekisababisha katika sekta ya utalii ni kikubwa sana," amesema Msigwa kupitia ukurasa wake wa Twitter.


Uwanja wa Ndege wa Arusha kwa siku sasa unapokea idadi kubwa ya ndege ambayo haijawahi kutokea.


Mbuga za wanyama na vivutio vikubwa vya watalii nchini, ikiwemo Ngorongoro, Serengeti, Kilimanjaro, Arusha, Zanzibar na kwingineko sasa kumefurika watalii hadi idadi ya hoteli na vyumba havitoshi.


"Kwa kweli hii haijawahi kutokea. sijawahi kuona idadi kubwa ya watalii namna hii Arusha tangu nizaliwe. Rais Samia anastahili pongezi kwa kutuletea neema hii kupitia Royal Tour," alisema Paul Mollel, dereva wa watalii jijini Arusha.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post