SERIKALI YATANGAZA KUTOA VITAMBULISHO VYA TAIFA 'NIDA' MILIONI 10


Mfano wa vitambulisho vya NIDA
Naibu Katibu Mkuu akizungumza kwenye kikao cha halmashauri kuu ya CCM wilaya Kigoma Vijijini akiwa kwenye ziara ya siku moja wilayani humo ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tano mkoani Kigoma.
Naibu Katibu Mkuu CCM Bara Christina Mndeme akihutubia mkutano wa hadhara kwenye kijiji cha Machazo kata ya Simbo Kigoma vijijini akiwa kwwnye ziara ya kichama mkoani Kigoma
Katibu wa CCM wilaya Kigoma Vijijini Rashidi Semindu Pawa (kulia) akitoa taarifa kwa Naibu Katibu Mkuu CCM Bara Christina Mndeme kuhusu hali ya siasa wilayani humo na malalamiko ya wananchi kuhusu changamoto ya upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii wakati Naibu Katibu Mkuu alipofanya ziara kutembelea wilaya hiyo. (Picha na Fadhili Abdallah)

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

Serikali imetangaza kuwa vitambulisho vya Taifa  milioni 10 vitaanza kutolewa kuanzia mwezi Januari mwaka 2023 ili kuhakikisha watanzania wote wanapata vitambulisho hivyo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Jumanne Sajini alitoa kauli hiyo ya serikali kwenye mkutano wa halmashauri kuu ya CCM wilaya ya Kigoma Vijijini kupitia simu ya mkononi ya Naibu Katibu Mkuu Bara, Christina Mndeme anayefanya ziara ya chama ya siku moja kwenye wilaya hiyo.


Sajini akijibu malalamiko ya wananchi wa wilaya hiyo waliowasilisha kwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM kwenye mkutano huo alisema kuwa tayari serikali imetenga shilingi bilioni 42 kwa ajili ya kushughulikia uchapaji na upelekaji wa vitambulisho hivyo kwa wananchi.

Alisema kuwa kuwepo kwa changamoto ya ugonjwa COVID ilikuwa moja ya sababu za kukwama kuchapishwa kwa vitambulisho hivyo kutokana na viwanda vya malighafi za kutengenezea vitambulisho kufungwa.

"Pia tulikuwa na changamoto ya mkataba na mkandarasi aliyepewa kazi ya kutengeneza vitambulisho hivyo lakini tumeshafikia sukuhisho na kazi itaanza mara moja,"alisema Naibu Waziri wa mambo ya ndani.

Alisema kwa sasa kuna vita vya Urusi na Ukraine pamoja na changamoto zilizopo watahakikisha mpango huo unafanyika kwa mafanikio na kazi iliyopo sasa ni kuwapatia namba wale wote ambao wameshasajiliwa kwenye mfumo waweze kuzitumia wakati wanasubiri vitambulisho.

Kufuatia kauli hiyo Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara,Christina Mndeme ameitaka wizara ya mambo ya ndani kupitia Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA) wanatekeleza kauli hiyo kwa vitendo ili vitambulisho hivyo viweze kutumika kwa matumizi yaliyokusudiwa.

Mndeme alisema kuwa suala la vitambulisho vya Taifa limekuwa lalamiko kuu la Taifa kwa wananchi hivyo ifike kwenye changamoto hiyo itatuliwe.


Awali Katibu wa CCM wilaya ya Kigoma Vijijini, Rashidi Semindu Pawa alisema kuwa upatikanaji wa namba za NIDA na vitambulisho vya Taifa ni moja ya malalamiko makubwa wanayopokea wanapofanya vikao na wananchi au kunapokuwa na ziara za viongozi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post