MIILI YA WALIOFARIKI KWENYE AJALI ILIYOUA WATU 20 KAHAMA YAENDELEA KUTAMBULIWA....HAYA HAPA MAJINA...YUMO FUNDI MAARUFU WA KAMERA LEONARD BASU

Leonard Basu enzi za uhai wake
Miili ya Watu 16, kati ya 20 ya waliofariki dunia kutokana na ajali ya magari matatu na trekta iliyotokea katika barabara ya Isaka - Kahama, kwenye eneo la kijiji cha Mwakata Wilayani Kahama mkoani Shinyanga imetambuliwa.


Ajali hiyo iliyotokea jana Agosti 8,2022 majira ya saa nne kasoro usiku ilihusisha magari matatu ikiwemo Hiace, Lori , gari ndogo aina ya IST na trekta.


Miongoni mwa abiria waliokuwa kwenye Hiace waliofariki dunia ni Fundi Maarufu wa Kamera Mjini Shinyanga Leonard Basu aliyekuwa anatokea Kahama kwenye semina ya Kanisa la Efatha.


Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Manispaa ya Kahama, Dkt. Deogratius Nyaga amethibitisha kupokea miili ya watu 20 kati yao wanaume waliofariki dunia 17, wanawake watatu na kwamba majeruhi 15.


Dkt. Nyaga amesema mpaka jioni ya leo miili ya marehemu 16 imetambuliwa ,9 imechukuliwa na ndugu, majeruhi 7 wanaendelea kupatiwa matibabu , wametoa rufaa kwa majeruhi wanne 4 na wengine wameruhusiwa kutoka hospitali.


Kaimu kamanda wa Polisi wa mkoa wa Shinyanga Leonard Nyandahu amesema, kati ya miili hiyo 16, miili ya marehemu 9 tayari imechukuliwa na ndugu kwa taratibu za mazishi na mingine 7 inasubiri taratibu za kifamilia.

Nyandahu amewataja Marehemu ambao wametambuliwa, kuwa ni Kano Lutema (48), mkazi wa Kahama, Jonas Kija (49), mkazi wa Kahama, Paul Choyo (23), mkazi wa Kahama na Tungu Magega (65),mkazi wa Kahama, Salinja Bukelebe (28), mkazi wa Kahama, Sarah Siti (46), mkazi wa Kahama, Nuhu Mpinga (28), mkazi wa Kahama na Augustino Mnyamba (28), mkazi wa Kahama.

Wengine ni Leonard Basu (52), mkazi wa Shinyanga, Musa Ally (25), mkazi wa Kahama, Sebastian Kimaro (28), mkazi wa Mwanza na Julius Jeremia (28) ambaye pia ni mkazi wa Mwanza, Erick Peter (31), mkazi wa Masumbwe, Flora Wilson (28) , mkazi wa Kahama, Aman Silus (35), mkazi wa Kahama na Nicolous Budole  (34), ambaye ni mkazi wa Didia Shinyanga.

Miili ya marehemu wanne mpaka sasa bado haijatambuliwa, na imehifadhiwa katika hospitali ya wilaya ya Kahama.


Soma Pia:

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments