SERIKALI KUWEKA MAZINGIRA MAZURI KWA WACHIMBAJI WADOGO


Waziri wa madini Dk. Doto Biteko (Kulia) akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini mkoani Kigoma. (Picha na Fadhili Abdallah)


Na Fadhili Abdallah,Kigoma

WAZIRI wa madini Dk. Doto Biteko amesema kuwa serikali inaziangalia sheria za madini na kuzifanyia marejeo ili kuwezesha wachimbaji wadogo kufanya kazi kwa ufanisi kuondokana na changamoto zinazowakabili. 

Waziri Biteko alisema hayo akizungumza na wachimbaji wadogo mkoani Kigoma na kusema kuwa Rais Samia ameshatoa agizo kuhakikisha wachimbaji wadogo hawasumbuliwi wala kunyanyaswa na kama kuna changamoto zitatuliwe kwa taratibu za vikao.


Biteko alisema kuwa wachimbaji wadogo wamekuwa na mchango mkubwa katika mapato ya nchi ambapo kwa mwaka uliopita serikali ilikusanya kiasi cha shilingi bilioni 620 kiwango ambacho hakijawahi kukusanywa kwa wachimbaji wadogo katika historia ya nchi hii.

“Kwa sasa wachimbaji wadogo katika mapato ya mwaka unaoishi Juni mwaka huu wachimbaji wadogo wamechangia asilimia 40 ya mapato wakishindana na wachimbaji wakubwa hivyo lazima serikali iweke mazingira ya kuwajali watu hapa,”alisema Waziri Biteko.

Kulingana na hali hiyo alisema kuwa ni lazima Tanzania iwe kitovu cha uwekezaji kwenye masuala ya madini kutokana na aina mbalimbali za madini zilizopo na namna serikali inavyoweka mazingira ambayo yanavutia wawekezaji kwenye madini.

Serikali inaungalia mkoa Kigoma kama moja ya maeneo ambayo uwekezaji kwenye madini unaweza kufanyika lakini bado ni kiasi kidogo sana cha madini ambacho kinachimbwa mkoani humo ukilinganisha na madini yaliyopo.

Kwa mwaka uliopita alisema kuwa mkoa umefanya biashara ya madini yenye thamani ya shilingi bilioni 14 ingawa utafiti wa kiwango cha madini kilichopo haujafanyika na hivyo utafiti utafanyika kujua wingi wa madini yaliyopi ili wawekezaji waweze kuwekekeza.

“Upo mradi wa uchimbaji wa NIKEL mkoa Kigoma lakini hakuna chochote ambacho kimefanyika kwa ajili ya uchimbaji wa madini hayo hivyo serikali inaanza mpango kuona namna gani uwekezaji utafanyika kwenye aina hii ya madini,”alisema.


Awali katibu wa Chama cha wachimba madini mkoa Kigoma, Lister Kalegeya akisoma risala ya wachimbaji wa mkoa huo kwa Waziri Biteko alisema kuwa wamekuwa wakifanya uchimbaji mdogo ambao haujui kiwango cha madini kilichopo hivyo kufanywa kwa utafiti kutakuwa na tija kwa uchimbaji wa madini mkoani humo.


Sambamba na hilo Kalegeya alisema kuwa masharti magumu ya upatikanaji wa mikopo kwa wachimbaji wadogo kumewafanya washindwe kufikia malengo yao katika uchimbaji na kufanya biashara ya madini yenye tija hivyo kuomba dhamana za mikopo ziangaliwe upya na serikali iweke udhamini ili wachimbaji hao waweze kukopesheka.


Kwa upande wake Afisa madini mkazi wa mkoa Kigoma, Pius Robe alisema kuwa mkoa Kigoma una aina mbalimbali za madini zinazochimbwa .

Afisa Madini Mkazi mkoa Kigoma Pius Robe akitoa taarifa ya mkoa mbele ya Waziri wa Madini Dk. Doto Biteko





Katibu wa Chama cha wachimba madini wadogo mkoa Kigoma Lister Kalegeya akisoma risala ya wachimbaji hao kwa waziri wa madini Dk. Doto Biteko mjini Kigoma.
Wachimbaji wadogo wa madini mkoa Kigoma wakimsikiliza Waziri wa Madini Dk. Doto Biteko mjini Kigoma

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments