TAMASHA LA MAJIMAJI SELEBUKA LAZINDULIWA, SERIKALI YASISITIZA KUHUSU MAADILI YA MTANZANIA


Serikali imesema kuwa imekamilisha uchapishaji wa kitabu cha mwongozo wa maadili na sasa inaendelea na kukusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusu maadili ya Mtanzania.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe Pauline Gekul wakati akizindua msimu wa 8 wa Tamasha la Majimaji Selebuka wilayani Songea, mkoani Ruvuma leo Julai 23,2022.

Amesema kuwa mchakato huo wa kukusanya maoni utakapokamilika serikali itakuja na mwongozo wa maadili ya Taifa ambao ni maelekezo yaliyotolewa na Mhe Rais, Samia Suluhu Hassan ili kuhakikisha vijana wa Kitanzania wanakuwa katika maadili sahihi.

“Mhe Rais ametupa kazi kubwa kuhakikisha tunakuja na mwongozo wa maadili wa Taifa letu. Kwa kiasi kikubwa sasa kumekuwa na mmomonyoko wa maadili katika nchi yetu. Wizara yetu tunakusanya maoni kwamba ni mambo gani ya kufanya na mambo gani hayapaswi kufanya.

Mhe Rais hafurahishwi na mmomonyoko wa maadili katika Taifa letu na hivyo tuna kazi ya kuwalea vijana wetu kwa kupitia matamasha kama haya ya utamaduni kujua tulipo toka na tulipo na pia kujua mila na destruri zetu zile zilizo nzuri.” amesema Naibu Waziri Gekul.

Naibu Waziri huyo pia alimpongeza Mbunge wa Songea Mjini ambaye pia ni Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe.Dk Damas Ndumbaro(Mb) kwa kuhakikisha tamasha hilo la Majimaji Selebuka linaendelezwa.

Kwa upande wake Mhe.Dk Ndumbaro amesema kuwa Tamasha hilo licha tuu ya kutoa burudani kwa wananchi pia ni sehemu ambayo watu wanaweza kujifunza tamaduni pamoja na mila za watu wa Ruvuma na pia wajasiriamali wanapata nafasi ya kuonyesha na kuuza bidhaa zao.

Pia Mhe.Dk.Ndumbaro ametoa wito kwa watu mbalimbali kuja kushuhudia tamasha hilo ambapo pia watapata nafasi ya kutembelea vivutio mbalimbali vilivyopo mkoani Songea Mjini na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.Tamasha hilo limehudhuriwa na Mhe.Fratei MassayMbunge wa Mbulu Vijijini na Mhe.Daimu Mpakate,Mbunge wa Tunduru.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post