PROGRAMU YA 'SUA STEP' MKOMBOZI WA UCHUMI KWA WANAFUNZI WA CHUO KIKUU CHA KILIMO SOKOINE (SUA)



Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Profesa Raphael Chibunda (wa kwanza kulia) akiwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam Profesa Boniventure Rutinwa (wa pilikulia) wakizungumza jambo walipokuwa wakiangalia Bidhaa za mbogamboga zilizozalishwa na wanafunzi wa SUA kwenye maonesho ya vyuo vikuu yanayofanyika Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Nyambilila Amuri Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Shahada za Awali SUA akizungumza na baandhi ya wanafunzi waliotembelea kwenye banda la chuo hicho katika maonesho ya vyuo vikuu Mnazi Mmoja.


Bi. Suzana Magobeko Afisa Mawasiliano na Masoko Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kilichopo mkoani Morogoro akifuatilia kwa makini wakati maofisa Udahili wa chuo hicho Mawesa Nicholaus kulia na Grace Kihombo wakiendelea na kudahili wanafunzi katika banda la chuo hicho


Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) Profesa Raphael Chibunda (wa tatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Chuo hicho kwenye Banda lao katika Maonesho hayo Jijini Dar es Salaam. PICHA ZOTE NA: HUGHES DUGILO


Na: Hughes Dugilo, DAR ES SALAAM.
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Shahada za awali Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Dkt. Nyambilila Amuri amesema kuwa kumekuwepo na muamko mkubwa kwa vijana kutaka kusoma masomo ya ujasiriamali hususani kilimo Biashara kutokana na fursa za kujikwamua kiuchumi zilizopo kwenye sekta hiyo.


Dkt. Nyambilila ameyasema hayo katika mahojiano maalum na waandishi wa habari katika Banda la Chuo hicho kwenye maonesho ya 17 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyofunguliwa rasmi Julai 17,2022 katika viwanja vya Mnazi mmoja Jijini Dar es Salaam.


Amesema kuwa katika kipindi cha hivi karibuni wameanzisha Programu ya Ujasiriamali ijulikanayo kama "SUA STEP" ambapo wanafunzi wanajiunga kwenye vikundi na kuanzisha Kampuni zao katika fani mbalimbali na kuweza kupata kazi za kutoa huduma mbalimbali ndani ya Chuo huku wakiendelea na masomo yao ambapo pia inawasaidia kujipatia kipato.

"Katika Programu hii wanafunzi tunawapa fursa ya kupata kazi ndani ya Chuo badala ya kutafuta watoa huduma nje ya Chuo, lakini kwa wale wanaofanya Kilimo tunawapa Vitalunyumba na eneo dogo la shamba kwaajili ya kuzalisha na kupata muda wa kuendelea na masomo yao"


"katika Programu hii tayari tumeshafanya usajili wa vikundi 10 vya wanafunzi ambavyo tayari wameanzisha Kampuni hizo ndani ya Chuo na wataweza kupata kazi za Kilimo, Tehama, kazi ya kuboresha utunzaji wa kumbukumbu, pia kuna kazi za kuweka mifumo mbalimbali ya umwagiliaji kama 'Drip Illigation' ambazo kazi zote hizo zitafanyika kama sehemu ya mafunzo lakini watakuwa wanalipwa" amesema Dkt. Nyambilila.


Naye Mmoja wa mnufaika wa Programu hiyo Mary Mosha amesema kuwa amenufaika na Programu hiyo ambayo yeye na wenzake walijikita kwenye kilimo biashara ambapo amesema kuwa fursa hiyo itamuwezesha kufanya shughuli za kilimo biashara kwa kuzalisha bidhaa zenye ubora unaokubalika kimataifa na kuongeza kuwa Chuo hicho kimewezesha kuwatafutia masoko ya bidhaa zao katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.


Kwa upande wake Afisa Mawasiliano na Masoko Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Suzana Magobeko ametoa wito kwa wananchi wote hususani vijana kujiunga na Chuo hicho ambacho kimejikita katika kutoa mafunzo na fani mbalimbli zitakazowasaidia kutoa ushindani katika soko la ajira na pia kujiajiri wenyewe katika shughuli zao za uzalishaji mali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post