WAKULIMA WAFUATE KANUNI ZA KILIMO CHA PAMBA KUKABILIANA NA WADUDU WAHARIBIFU


Mkazi wa kijiji cha Ipumbulya kata ya Bukoko wilaya ya Igunga mkoani Tabora akiwa amebeba pamba akiipeleka kuuza kwenye  Chama cha Msingi cha Ushirika (AMCOS) ya Segagi Balimi kijiji cha Ipumbulya kata ya Bukoko wilaya ya Igunga

Na Kadama Malunde  - Malunde 1 blog

Wakulima wa  zao la pamba wameshauriwa kuzingatia kanuni za kilimo ikiwemo kupulizia dawa za kuua wadudu wanaoshambulia zao hilo ili kuondokana na malalamiko ya kwamba dawa haziui wadudu na kuachana na tabia ya kusubiri hadi waone wadudu shambani ndipo wapulizie dawa.


Ushauri huo umetolewa na Afisa Kilimo Mwandamizi na Mkaguzi wa Pamba wilaya ya Igunga, Venance Kankutebe na  Afisa Mkaguzi wa pamba wilaya ya Nzega mkoani Tabora, Azaria Sanga wakati wa ziara ya Maafisa Mawasiliano wa Wizara ya Kilimo wakitembelea wadau wa pamba mkoani Tabora.


Afisa Kilimo Mwandamizi na Mkaguzi wa Pamba wilaya ya Igunga, Venance Kankutebe amesema ni vyema wakulima wakafuata kanuni za kilimo ikiwemo kuzingatia matumizi sahihi ya viuatilifu na vipulizi kwa wakati mara tum mea unapoota na kuachana na tabia ya kupulizia dawa baada ya kuona wadudu.


“Tunaendelea kutoa elimu kwa wakulima juu ya matumizi sahihi ya viuatilifu na vipulizi na katika msimu ujao tumejipanga kikamilifu kutoa viuatilifu na mbegu mapema”,amesema Kankutebe.


“Tumejipanga kukabiliana na mdudu Chawajani, Vidung’ata na vidukali kwani hawa ni wadudu hatari kwenye mmea wa pamba kwa sababu wananyonya maji maji yaliyopo kwenye pamba na kufanya mmea udhoofike na  kusababisha uzalishaji wa pamba ushuke”,ameeleza Kankutebe.

Naye Afisa Mkaguzi wa pamba wilaya ya Nzega mkoani Tabora, Azaria Sanga pia amesisitiza wakulima kuacha tabia ya hadi waone wadudu ndipo wachukue hatua ya kupulizia dawa ili kukabiliana na wadudu wanaoshambulia pamba huku akiwasihi kutumia jembe la palizi  linalolokokotwa na ng’ombe ambalo linaongeza tija kwenye kilimo.

“Tunawashauri wakulima kuchangamkia majembe ya palizi. Jembe la palizi lina faida nyingi ikiwemo kupunguza gharama na muda wa kupalilia shamba. Majembe ya palizi  yanapatikana Bodi ya pamba na kwa wanaohitaji majembe haya wawasiliane na maafisa kilimo wa kata husika na wao watawasilisha majina bodi ya pamba. Lakini pia tunashauri Wakulima wakiona teknolojia za kisasa katika kilimo wachangamkie ili kuongeza tija”,amesema.


Sanga ametumia fursa hiyo kuwataka vijana kuchangamkia kilimo kwani kilimo siyo adhabu wala siyo utumwa bali kuna utajiri mkubwa wa kumbadilisha mtu kiuchumi na kubadilisha maisha yake na kuongeza mapato ya nchi akisisitiza kuwa hivi sasa kilimo kinalipa na ni biashara.


Katibu wa Chama cha Msingi cha Ushirika (AMCOS) ya Segagi Balimi kijiji cha Ipumbulya kata ya Bukoko wilaya ya Igunga, Sendama Lutema na Mhasibu wa AMCOS ya Mbogwe wilayani Nzega, Shija Madimi wamesema miongoni mwa changamoto walizokutana nazo katika msimu huu ni wadudu waharibifu wa pamba.


Wamesema wadudu hao akiwemo mdudu hatari chawajani wamekuwa hawafi wanapopuliziwa dawa hali inayoshusha uzalishaji wa pamba na kuomba serikali kuleta dawa kali zaidi ili kukabiliana na wadudu hao.

Hata hivyo  wamesema katika msimu huu pamba ni safi na bei imekuwa ya kuridhisha kwani inauzwa si chini ya bei elekezi ya serikali ambayo ni shilingi 1560/= na wanaendelea kukusanya pamba kutoka kwa wakulima.

Afisa Kilimo Mwandamizi na Mkaguzi wa Pamba wilaya ya Igunga, Venance Kankutebe akiwashauri wakulima kuzingatia kanuni za kilimo cha pamba ili kukabiliana na wadudu waharibifu.
Katibu wa Chama cha Msingi cha Ushirika (AMCOS) ya Segagi Balimi kijiji cha Ipumbulya kata ya Bukoko wilaya ya Igunga, Sendama Lutema akielezea kuhusu kilimo cha pamba
Muonekano wa sehemu ya pamba katika ghala la  Chama cha Msingi cha Ushirika (AMCOS) ya Segagi Balimi kijiji cha Ipumbulya kata ya Bukoko wilaya ya Igunga
Afisa Mkaguzi wa pamba wilaya ya Nzega mkoani Tabora, Azaria Sanga akielezea kuhusu kilimo cha pamba
Mhasibu wa Chama cha Msingi cha Ushirika (AMCOS) Mbogwe wilayani Nzega, Shija Madimi akielezea kuhusu kilimo cha pamba
Muonekano pamba za mfano katika Chama cha Msingi cha Ushirika (AMCOS) Mbogwe wilayani Nzega
Balozi wa zao la Pamba nchini Aggrey Mwanri akionesha jembe la palizi kwa ajili ya zao la pamba na mazao mengine
Balozi wa zao la Pamba nchini Aggrey Mwanri akielezea kuhusu jembe la palizi kwa ajili ya zao la pamba na mazao mengine.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments