WANANCHI WATAKIWA KUTUNZA MAZINGIRA ILI KUEPUKA MABADILIKO YA TABIA NCHI


Mstahiki meya wa Jiji la Arusha Maximilian Iranghe akiwa na mkurugenzi wa bonde la Mto Pangani Segule Segule katika uzinduzi wa uwekaji mipaka katika hifadhi ya vyanzo vya maji jiji Arusha.

Na Rose Jackson - Arusha

Wananchi mkoani Arusha wametakiwa kutunza mazingira pamoja na vyanzo vya maji ikiwa ni pamoja na kukaa umbali wa mita 60 kutoka kwenye vyanzo hivyo ili kuepuka athari za uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.

Akizungumza leo katika uzinduzi wa kampeni ya uwekaji wa mipaka(Beacons) katika hifadhi ya vyanzo vya maji jijini Arusha, meya wa halmashauri ya Jiji la Arusha Maximilian Iranqhe alisema kuwa wananchi wanapaswa kutunza vyanzo vya maji ili viweze kuwa endelevu kwa vizazi vijavyo.


Iranqhe amesema ili kuhifadhi vyanzo vya maji Wananchi wanapaswa kuepuka kufanya shughuli za kibinadamu pembezoni mwa vyanzo hivyo ikiwemo ujenzi wa nyumba na makazi ili kuepuka mabadiliko ya tabia nchi.


Aidha amewataka maafisa mipango miji kujitafakari namna ya wanavyotoa vibali vya ujenzi kwa wananchi kwa kuwa utoaji holela wa vibali umekuwa ukichangia uharibifu wa vyanzo vya maji


Mkurugenzi wa bodi ya maji bonde la mto Pangani, Segule Segule amesema uwekaji wa alama za mipaka katika hifadhi ya vyanzo vya maji husaidia kufahamisha wananchi kuwa wanapaswa kukaa nje ya mita 60 kutoka kingo za vyanzo vya maji.


"ili kuhakikisha vyanzo vya maji vinakuwa endelevu ni lazima tuanzie katika vyanzo husika na kusimamia kwa lengo la kuhakikisha hayaleti madhara kwa watu na Kwa vizazi vijavyo",aliongeza Segule.


Segule Segule alisema zoezi hilo la uwekaji alama limeanza katika mto Naura lengo ni pamoja na kuhamasisha utunzaji wa vyanzo vya maji ikiwa shughuli za binadamu zikitakiwa kufanyika nje ya mita 60.

Kwa upande wake Afisa mazingira kutoka bodi ya maji bonde la mto Pangani,Felista Joseph alisema matatizo yaliyopo katika mto Naura ni pamoja na shughuli za kibinadamu,ujenzi wa makazi ya watu katika eneo la chanzo cha mto Naura na utupaji wa taka ovyo katika mto huo.


"Shughuli mbalimbali za biandamu zimekuwa zikiathiri ubora wa maji hivyo uwekaji wa alama hizo zitakwenda kuondoa baadhi ya matatizo hayo na iwapo mtu anapokiuka sheria atapata adhabu kwa mujibu wa kanuni",alibainisha.


Naye Afisa Mazingira kutoka Baraza la taifa la hifadhi na usimamizi wa mazingira Kanda ya Kaskazini Francis Nyamhanga alisema ili kuwa na vyanzo vya maji ni jukumu la kila mmoja kutunza mazingira na kueleza Mikakati waliyoweka ili kutunza mazingira kuwa ni kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira na kushiriki katika shughuli mbali mbali za usafi katika kuazimishwa wiki hii ya mazingira duniani.


Hata hivyo uwekaji wa alama za mipaka (Beacons) katika hifadhi ya vyanzo vya maji jiji la Arusha umeanza katika mto Naura na itafuatiwa na mto Ngarenaro, Themi na mto Kijenge.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments