GEITA GOLD FC YATEMBELEA MIRADI INAYOFADHILIWA NA GGML


Kutoka kushoto Stephen Mhando, Meneja Uhusiano na Mawasiliano kwa umma kutoka GGML; Manace Ndoroma, Meneja Mwandamizi wa masuala ya ubia -GGML; Msimamizi wa ASM wa AngloGold Ashanti, Siguiri Guinea, Mamoudou Berete na Afisa Maendeleo ya Uchumi wa Jamii wa GGML, Regina Mabula wakikagua maendeleo ya ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu mjini Geita.
Kocha Mkuu wa Klabu ya Geita Gold FC, Fred Felix ‘Minziro’ (kulia) na Meneja Mwandamizi wa masuala ya ubia kutoka GGML, Manace Ndoroma (kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na GGML kupitia mpango wa Uwajibika wa Kampuni kwa jamii (CSR).
Timu ya Geita Gold Football wakiwa katika picha ya pamoja na watoto wanaolelewa katika Kituo cha Moyo wa Huruma, wafanyakazi wa GGML na viongozi wa halmashauri ya Mji wa Geita.


Na Mwandishi wetu

Timu ya mpira wa miguu ya Geita Gold Football Club inayofadhiliwa na Kampuni ya GGML imetembelea miradi ya jamii inayofadhiliwa na kampuni hiyo kupitia mpango wake wa huduma kwa jamii.


Akizungumza wakati wa ziara ya timu hiyo, Meneja Mwandamizi anayehusika na ubia kutoka GGML, Manace Ndoroma amesema kuwa pamoja na kutoa udhamini wa shilingi za Kitanzania milioni 500 kwa timu hiyo, wameamua kuikaribisha timu hiyo kuona uwekezaji unaofanywa na kampuni ya GGML katika jamii ya Geita.


“Tumefarijika sana kuwa wadhamini wakuu wa timu ya Geita Gold Football Club kwa sababu jitihada zao za kupanda katika msimamo wa ligi kuu zimeongeza chachu ya michezo kwa mkoa wetu wa Geita. Timu hii sasa imekuwa balozi wetu mzuri anayetutangaza sisi GGML, Mji wa Geita na mkoa wetu kwa ujumla,” alisema Bw Ndoroma.


Afisa Mtendaji mkuu wa timu ya Geita Gold Football Club Bw Simon Shija ameipongeza kampuni ya GGML kwa kuendelea kuinufaisha jamii ya Geita kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo.


“Watu wengi wanaisifia timu yetu kwa kufanya vizuri katika msimamo wa ligi. Lakini siri ya mafanikio yetu ni pamoja na kushikwa mkono na wadau mbalimbali wakiwemo GGML ambao pamoja na kutupatia udhamini mkuu, wanatujengea uwanja wa mpira wa kisasa Mjini Geita. Ni matumaini yetu kuwa hata tutakapokuwa tunacheza mechi ngumu dhidi ya timu za Simba, Yanga hapa mjini Geita, mashabiki wetu wa ndani na nje ya Geita watafurahia na kutushangilia kutokana na uwekezaji wa GGML ndani ya mji huu (Geita). Pia tunatoa rai kwa wadhamini wengine waendelee kutushika mkono, kwani timu yetu inatamani kuendelea kufanya vizuri zaidi kwenye msimu ujao,” alisema Bw Shija.


Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita Bw. Lee Joshua ameipongeza GGML kwa kuendelea kuwekeza kwenye jamii katika halmashauri yake kwa wakati, hatua inayorahisisha utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo yenye tija katika jamii.


“Halmashauri yetu ya Mji Geita, imekuwa mnufaika wa uwekezaji mkubwa kwenye miradi ya jamii. Mojawapo ya matunda ya uwekezaji huo ni utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi wa soko la Dhahabu, soko la Katundu, barabara za lami pamoja na kituo cha uwekezaji cha EPZA: miradi ambayo timu yetu ya mpira ya Geita Gold Footaball Club imetembelea leo. Pia, tunafurahia kutembelea miradi hii pamoja na timu yetu ya mpira ambayo kwa kiasi kikubwa imeweza kutangaza vivutio vya Mkoa wa Geita, zikiwemo sehemu za utalii,” alisema Bw. Lee Joshua.


Katika ziara hiyo, timu ya Geita Gold Football Club ilipata pia fursa ya kuwafariji na kupata nao chakula cha mchana watoto yatima wa kituo cha Moyo wa Huruma kinachofadhiliwa na GGML kupitia mradi wake wa Kili Challenge.


GGML imekuwa kinara wa uwekezaji kwenye jamii tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000 ambapo vipaumbele vikuu vimekuwa ni miradi ya elimu, afya, maji, barabara, miradi ya kukuza kipato na miradi mingine mingi ya kijamii ili kuhakikisha jamii mwenyeji inapata maisha bora. Mapema mwaka huu, GGML iliibuka mshindi wa jumla katika kampuni zinazofanya vizuri kwenye sekta ya madini nchini Tanzania kwa mwaka 2020/2021 baada ya kunyakua tuzo katika vipengele vya uwajibikaji wa kampuni kwa jamii, mazingira, usalama, mlipaji bora wa mapato (kodi) na uendelezaji wazawa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments