OFISI YA TAIFA YA TAKWIMU YAWATAHADHARISHA WANAOSAMBAZA TAARIZA ZA UONGO KUHUSU SENSA

Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt.Albina Chuwa akiongea na waandishi wa habari (Hawapo pichani)kuhusu taarifa za uzushi zinazo zagaa mitandaoni kuhusu sensa ya watu na makazi na kusema kuwa taarifa hizo zina lengo la kukwamisha zoezi hilo.

Na  Dotto Kwilasa,DODOMA

SERIKALI kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu imewatahadharisha wanaosambaza taarifa za uongo zinazohusu sensa ya watu na makazi  kwenye mitandao ya kijamii huku ikikanusha kuwa taarifa hizo si rasmi ambazo zimekwenda mbali na kubatilisha tarehe ya usajili kuwa ni 29Mei,2022 badala ya 02,Juni,2022.

Hatua hiyo imekuja kufuatia kuwepo kwa taarifa zisizo rasmi zinazo sambaa mitandaoni kuhusu orodha ya majina ya makarani yenye kichwa cha habari “Orodha ya majina ya maombi ya kazi ya muda ya sensa ya watu na makazi yaliyohakikiwa na kujibiwa kikamilifu”.

Akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dodoma,Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt.Albina Chuwa amewataka watanzania kupuuza taarifa hizo na kuongeza kuwa mchakato wa ajira za muda za makarani na wasimamizi wa sense bado unaendelea .

“Niwaombe watanzania wapuuze uongo na taarifa nyingine zinazohusu sensa ambazo sio rasmi kwani watu hawa hawana nia njema na Serikali  na watanzania kwa ujumla,mchakato bado unaendelea katika ngazi ya kata/shehia na halmashauri zote,”amesema Dkt.Chuwa

Amefafanua kuwa zoezi la uchambuzi wa maombi kwa waombaji wote linatarajiwa kuanza 02,Juni,2022 kwenye kila kata au shehia husika baada ya kukamilika kwa mafunzo ya maafisa watakao husika kufanya usaili .

Mbali na hayo  amesema mchakato wa ajira za makarani na wasimamizi wa sense linakwenda vizuri kulingana na ratiba ya sense inayotarajiwa kufanyika ifikapo 23,Agosti,2022 .

“Naomba mfikishe ujumbe huu kwa watanzania wote kwamba taarifa yoyote inayohusu mwenendo wa maandalizi ya sensa ya watu na makazi ,sensa ya majengo na sensa ya anwani za makazi ikiwemo ajira hizi za muda itatolewa na serikali kupitia vyombo vya habari na si vinginevyo,”amesisitiza Mtakwimu huyo wa Serikali

Mnamo tarehe 05,Mei,2022,Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitangaza rasmi kuanza kupokea maombi ya kazi za muda za makarani na wasimamizi wa sensa ya watu na makazi ifikapo 23,Agosti,2022 kupitia mfumo wa maombi wa kielekroniki.

Muda wa maombi hayo ulifikia tamati tarehe 19,Mei,2022 ambapo idadi ya waombaji ilifikia 689,935 kati ya 205,000 wanaohitajika kwenye zoezi hilo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post