MTAKWIMU MKUU WA SERIKALI ATAKA WAOMBAJI WA KAZI ZA MUDA KUJAZA TAARIFA ZAO KWA USAHIHI


***************************

Na Dotto Kwilasa,DODOMA

SERIKALI kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS)imesema mwenendo wa uombaji wa kazi za muda za makarani na wasimamizi wa Sensa ya Watu na Makazi linaendelea vizuri ambapo hadi Mei 9 mwaka huu watu 119,468 wameomba.

Akizungumza na wandishi wa habari jana jijini hapa Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk.Albina Chuwa alisema kati ya waombaji hao 46,159 ni waajili kutoka sekta ya umma na binafsi.

Amesema waombaji wengine 14,393 wamejiajiri katika sekta mbalimbali na waombaji 58,916 ni wale ambao hawana ajira yoyote.

"Mei 5 mwaka huu serikali ilitangaza rasmi kuanza kupokea maombi ya kazi za muda za makarani na Wasimamizi wa sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 23 mwaka huu kupitia mfumo wa kielekroniki mwenendo wa uombaji unaendelea vizuri nchi nzima,"amesema

Dk.Albina amesema kuna baadhi ya changamoto ambazo waombaji wamekuwa wakikumbana nazo ikiwemo kutokujaza taarifa sahihi kama barua pepe na namba za simu na hivyo kushindwa kupokea neno la siri na taarifa nyingine muhimu.

Ametaja changamoto nyingine kuwa ni waombaji kusahau jina la mtumiaji na neno la siri hivyo kushindwa kuhuisha fomu namba moja iliyoidhinishwa na mwajiri kwa waajiriwa na viongozi wa serikali za mitaa ikiwa ni pamoja na baadhi ya waombaji kukosa baadhi ya taarifa kama vile Namba ya Kitambulisho Cha Taifa(NIDA) na Cheti cha Kuzaliwa.

"Waombaji wote wanatakiwa kuwa makini wakati wa kuingia katika mfumo na kusoma maelekezo kabla ya kuanza kujaza fomu na kuhakikisha taarifa zinajazwa kwa usahihi kuondoa usumbufu wa kuhuisha taarifa mara kwa mara,wanatakiwa kujaza namba ya simu na barua pepe ambayo inatumika wakati wote ili aweze kupokea taarifa za akaunti yake ya kuingia katika mfumo mapema iwezekanavyo,"anasisitiza.

Pamoja na hayo amewataka waombaji hao pia kuandaa viambatisho muhimu kama cheti cha kuzaliwa,cheti cha kidato cha nne na namba ya NIDA ili wakati wa kujaza fomu wasikwame na kwamba maombi hayo ya kazi ya sensa yanapatikana bila malipo.

"Nawasisitiza waombaji wote wanatakiwa kutuma maombi kabla ya mei 19 mwaka huu saa sita usiku,ni muhimu kwenda na wakati ,lazima Kila mmoja wetu atambue umuhimu wa sensa na kuwajibika ipasavyo,"amesema

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments