WANAFUNZI WAKUMBWA NA VITENDO VYA ULAWITI ,TABIA CHAFU MWANZA...KIVULINI YATAKA NGUVU ZA PAMOJA KUKOMESHA


Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la KIVULINI, Yassin Ally akizungumza kwenye kikao cha wadau kilichofanyika Kata ya Mirongo jijini Mwanza kwa lengo la kujadili na kuweka mikakati ya kutokomeza ukatili wa kijinsia hususani kwa watoto na wanawake.

***

Imeelezwa kuwa vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ulawiti vimeshamiri katika Kata ya Mirongo jijini Mwanza huku wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari wakiwa wahanga wakubwa wa vitendo hivyo viovu na vya udhalilishaji.


Licha ya kukosekana takwimu rasmi, lakini vitendo hivyo vinadaiwa kufanywa na baadhi ya wananchi ambao wamekuwa wakiwalaghai wanafunzi huku vingine vikifanywa na wanafunzi wenyewe ambapo baadhi ya wahanga wametajwa kutoka Shule za Msingi Mirongo na Nyanza pamoja na Shule ya Sekondari Mirongo.


Kutokana na changamoto hiyo, shirika la kutetea haki za wanawake na watoto la KIVULINI limelazimika kuwakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi dini, serikali, wazazi pamoja na walimu wakuu kutoka Kata ya Mirongo ili kujadili na kuweka mikakati ya kukabiliana na vitendo hivyo.


Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mirongo, Edna Kidudo ameshauri kuwekwa uzio kwenye Shule hiyo ili kuimarisha usalama wa wanafunzi pamoja na kudhibiti tatizo la wanafunzi kutoroka shuleni wakati wa masomo huku Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyanza, Liberata Lubasha akitoa rai kwa Serikali kuweka mkakati wa kuzuia biashara holela zinazofanywa katika maeneo ya Shule kwani zinachochea vishawishi kwa wanafunzi.


"Uwepo wa baa katika eneo la Shule ni hatari kwa usalama na ustawi wa wanafunzi, tumejaribu mara kadhaa kuwasiliana na mamlaka zinazohusika ili ziweze kuondoa baa hii bila mafanikio, uwepo wa baa hii ni hatari make wateja wake wengi ni wanafunzi wetu” alisema mwalimu Liberata akielezea changamoto ya uwepo wa baa jirani na Shule ya Msingi Nyanza.


Naye Sheikh wa Msikiti wa Mabanzi ulioko Mtaa wa Uhuru jijini Mwanza, licha ya kulaani vitendo vya udhalilishaji dhidi ya wanafunzi, pia ameomba serikali kuchukua hatua stahiki za kisheria kwa watu wanaohusika na vitendo vya Ukatili wa Kijinsia.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la KIVULINI, Yassin Ally amehimiza ushirikiano wa viongozi wa dini, serikali pamoja na jamii katika kutokomeza vitendo vya ulawiti kwa wanafunzi, utoro, ulevi pamoja na matumizi ya dawa za kulevya miongoni mwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari jijini Mwanza.


Mkaguzi wa Polisi Kata ya Mirongo, Fatuma Mpinga amesema ni vyema wanajamii wakashiriki katika suala la ulinzi shirikishi katika maeneo yao hatua itakayosaidia kupambana na vitendo vya uhalifu na ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto na wanawake.


Kando na hayo, Afisa Mtendaji Kata ya Mirongo, Simon Fulko ametoa rai kwa wakazi wa Kata hiyo kushiriki kikamilifu katika zoezi la sensa ya watu na makazi litakalofanyika nchini Agosti 23, 2022 kwani ni muhimu ili kuwezesha upatikanaji wa takwimu zitakazotumika kwa ajili ya mipango ya maendeleo.
#BMGHabari
Afisa Mtendaji Kata ya Mirongo, Simon Fulko (katikati) akizungumza kwenye kikao hicho. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji Shirika la KIVULINI, Yassin Ally na kulia ni Mkaguzi wa Polisi Kata ya Mirongo, Fatuma Mpinga.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Rufiji jijini Mwanza, Abdillah Mbarak akichangia hoja kwenye kikao hicho.
Mkaguzi wa Polisi Kata ya Mirongo, Fatuma Mpinga akizungumza kwenye kikao hicho.
Sheikh wa Msikiti wa Mabanzi ulioko Mtaa wa Uhuru jijini Mwanza, Khalifa Mussa akitoa nasaha zake kwenye kikao hicho.
Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Nyanza jijini Mwanza, Mwl. Liberata Lubasha akichangia mada kwenye kikao hicho.
Mmoja wa washiriki wa kikao hicho kutoka kundi la waendesha bodaboda akichangia hoja.
Katika kikao hicho, wazazi na walezi wametakiwa kufuatilia kwa ukaribu mienendo ya watoto wao kuanzia nyumbani hadi shuleni hatua itakayosaidia kuwakinga na vitendo hatarishi ikiwemo ulawiti.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments