DC MBONEKO AONYA MATUMIZI FEDHA ZA MFUKO WA JIMBO, WAKANDARASI WAZINGUAJI...ATAKA USHIRIKIANO MADIWANI NA WATENDAJI


 
Mkuu wa wilaya ya Shinayanga Jasinta Mboneko akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani Manispaa ya Shinyanga.


Na Marco Maduhu, SHINYANGA

MKUU wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, ameshiriki kwenye kikao cha Baraza la Madiwani Manispaa ya Shinyanga, na kutoa maelekezo ya utendaji kazi kwa ajili ya mustakabali wa maendeleo ya Manispaa hiyo.

Baraza hilo la Madiwani Manispaa ya Shinyanga, limehitimishwa leo Mei 11, 2022, ambalo lilianza jana Mei 10 kwa ajili ya kujadili ajenda mbalimbali.

Mboneko akizungumza kwenye Baraza hilo la Madiwani, amewaomba Madiwani watoe ushirikiano kwa watendaji wa Serikali, ili wafanye kazi pamoja na kuleta maendeleo.

“Waheshimiwa madiwani muwape ushirikiano watendaji wetu wa Serikali, kuna baadhi ya Kata nimeshaanza kusikia malalamiko, hamuwapi ushirikiano,”alisema Mboneko.

“Lakini pia wapo watendaji wetu ambao hawafanyi vizuri, nimeshamwambia Mkurugenzi aanze kuchukua hatua, na kuna maeneo mengi Mstahiki Meya tulienda Madiwani wanawakataa watumishi hadharani mbele ya mkutano wa wananchi,”aliongeza.

Aidha, aliwataka pia Madiwani na wataalum waende kwenye miradi, na kusimamia miradi hiyo itekelezwe kwa ubora unaotakiwa na kwa wakati, pamoja na kutoa taarifa za miradi hiyo kwa maofisa Tarafa kwa kuwa nakala na wananchi kuwapatia taarifa za fedha za miradi hiyo.

Mboneko alionya pia fedha za mfuko wa jimbo marufuku kuzibadilishia matumizi bali zielekezwe kwenye miradi husika.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa wilaya, ametoa maagizo kwa wenyeviti wote wa Serikali za Mitaa vijiji, vitongoji na kwenye Kata, wasome mapato na matumizi kwa wananchi, ili kuondoa malalamiko na wajue zimekusanywa fedha kiasi gani na zimetumikaje.

Alizungumzia pia suala la Tozo za Maegesho ya Magari, ambalo kwa sasa limerudi chini ya Halmashauri na kutoka (TARURA), na kutaka usimamizi mzuri wa ukusanyaji wa fedha hizo na kuongeza mapato ya Halmashauri.

Akizungumzia zoezi la uwekaji Anwani za makazi ametaka liendelee na hadi kufikia mwisho mwa Mei liwe limekamilika ili kuendelea kulinda heshima ya Shinyanga kuongoza kitaifa katika zoezi hilo.

Mboneko alizungumzia pia suala la Wakandarasi ambao wanasua sua kutekeleza ujenzi wa miundombinu ya barabara, kuwa ameshakaa na Wakandarasi hao Jumatatu iliyopita na kuwaeleza kuwa hadi kufikia mwisho mwa mwezi huu barabara zote zikamilike na waliopitiliza muda wakatwe fedha zao.

Awali Madiwani wakizungumza kwenye kikao cha Baraza hilo, walilalamikia tatizo la kupewa Wakandarasi wasio na sifa ambao hawana uwezo wa kutengeneza barabara na kusababisha Manispaa hiyo kukabiliwa na ubovu mkubwa wa barabara.

Mmoja wa madiwani hao Rubeni Dotto kutoka Lubaga, alisema maeneo mengi ya Manispaa ya Shinyanga miundombinu yake ya barabara ni mibovu, na hiyo inasababishwa kupewa kazi Wakandarasi wasio na uwezo, na hawana vifaa vya utengenezaji wa barabara hizo hadi wakodi.

Naye Diwani wa Kitangili Mariamu Nyangaka, alisema Wakandarasi ambao wamepewa katika Manispaa hiyo hawafai, kwa sababu hadi sasa unakaribia mwaka mwingine wa fedha (2022-2023), lakini hakuna matengenezo yoyote ya barabara ambayo yamefanyika.

“Matengenezo ya miundombinu ya barabara ni bajeti ya mwaka wa fedha (2021-2022), lakini hadi sasa tunakwenda kwenye mwaka mwingine wa wa fedha(2022-2023),wakandarasi hawajafanya chochote sababu hawana uwezo, na kusababisha barabara kuendelea kuwa mbovu,”alisema Nyangaka.

Diwani wa Kizumbi Reuben Kitinya, alitupia lawama suala kutoa kazi kwa Wakandarasi kwa kutumia mfumo, ambao baadhi wamekuwa wakijaza kuomba kazi kwa kutumia mfumo huo na kusababisha Manispaa hiyo kupewa Wakandarasi wasio na uwezo.

Kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Shinyanga Elias Masumbuko, aliwataka wakala hao wa barabara mjini na vijini (TARURA), wawajibike ipasavyo kuwabana Wakandarasi kutengeneza miundombinu ya barabara, kwa kufuata mipango kazi yao kwa mujibu wa mikataba, ili wanaposhindwa kuwajibika ipasavyo iwe virahisi kuwachukulia hatua kisheria.

Meneja Wakala wa Barabara mjini na vijijini (TARURA) wilaya ya Shinyanga Mhandisi Samson Pamphili, alikiri Wakandarasi ambao wamepewa kazi za matengezo ya barabara katika Manispaa hiyo ya Shinyanga hawana uwezo, na hiyo imesababishwa kuomba kazi kupitia mfumo, na hata uwezo wao wa kukodi mitambo ni mdogo.

Aidha, alisema malalamiko yote ambayo yametolewa na madiwani kwenye kikao hicho cha baraza, ameyachukua na atayafikisha ngazi za juu ili yafanyiwe kazi.

Meneja huyo alisema kuwa katika mwaka wa fedha (2021-2022) walitengewa kiasi cha fedha Sh.bilioni 2.5, fedha za matengenezo ya barabara ni Sh. bilioni 1.5, fedha mfuko wa jimbo Sh.milioni 500, tozo za mafuta Sh.milioni 500, na mpaka sasa wameshapokea kiasi cha fedha Sh,bilioni 2 sawa na asilimia 78.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani Manispaa ya Shinyanga.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Jomaary Satura, akisoma taarifa ya kwenye kikao cha Baraza la Madiwani.

Meya wa Manispaa ya Shinyanga Elias Masumbuko akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani Manispaa ya Shinyanga.

Kikao cha Baraza la Madiwani Manispaa ya Shinyanga kikiendelea.

Madiwani wa Manispaa ya Shinyanga wakiwa kwenye kikao cha Baraza.

Madiwani wa Manispaa ya Shinyanga wakiwa kwenye kikao cha Baraza.

Madiwani wa Manispaa ya Shinyanga wakiwa kwenye kikao cha Baraza.

Madiwani wa Manispaa ya Shinyanga wakiwa kwenye kikao cha Baraza.

Madiwani wa Manispaa ya Shinyanga wakiwa kwenye kikao cha Baraza.

Madiwani wa Manispaa ya Shinyanga wakiwa kwenye kikao cha Baraza.

Madiwani wa Manispaa ya Shinyanga wakiwa kwenye kikao cha Baraza.

Madiwani wa Manispaa ya Shinyanga wakiwa kwenye kikao cha Baraza.

Madiwani wa Manispaa ya Shinyanga wakiwa kwenye kikao cha Baraza.

Wataalam wakiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani.

Wataalam wakiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani.

Wataalam wakiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani.

Wataalam wakiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani.

Na Marco Maduhu, SHINYANGA.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments