SERIKALI KUANZA KUTEKELEZA MPANGO WA HEDHI SALAMA KWA WASICHANA NA WANAWAKE


Mke wa Makamu wa Raisi Mama Mbonimpaye Philip Mpango (katikati mwenye kilemba cha Bluu) akitembelea mabanda ya maonyesho ya bidhaa mbalimbali za hedhi salama wakati wa maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya hedhi salama yaliyofanyika mkoani Kigoma. (Picha na Fadhili Abdallah)
Baadhi ya wananchi wa manispaa ya Kigoma Ujiji wakipata maelezo kuhusu matumizi sahihi ya taulo za kike zenye ubora wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya hedhi salama yaliyofanyika Kitaifa mkoani Kigoma.
Wadau kutoka taasisi na mashirika yanayojihusisha na masuala ya utu mwanamke wakionyesha taulo za kike wakati wa maadhimisho ya siku ya hedhi yaliyofanyika kitaifa mkoani Kigoma mei 28 mwaka huu.
Mke wa Makamu wa Raisi wa Tanzania Mama Mbonimpaye Philip Mpango (katikati mwenye kilemba cha Bluu) akiongoza wake wa viongozi wa serikali na viongozi wa serikali wanawake wa mkoa Kigoma kupiga picha wakati wa maadhimisho ya siku ya hedhi salama ambayo kitaifa yalifanyika mkoani Kigoma.


Na Fadhili Abdallah,Kigoma

SERIKALI imetangaza kuwa imeanza kutekeleza mpango wa kuondoa changamoto ya upatikanaji wa taulo za kike kwa wanafunzi wa ngazi zote nchini ili ifikapo mwaka 2030 suala la hedhi isiwe kikwazo kwa wanafunzi hao kutimiza malengo yao kwenye maendeleo .

Katibu Mkuu wa wizara ya afya,Profesa Abel Makubi alisema hayo katika siku ya kimataifa ya hedhi duniani ambayo kitaifa ilifanyika mkoani Kigoma na kusema kuwa serikali inaandaa mwongozo ambao utawezesha kuwepo kwa hedhi salama na wanafunzi wote wanatekeleza mipango yao bila wasiwasi wanapokuwa kwenye siku zao.

Akimwakilisha Waziri wa afya,Dk.Dorothy Ngwajima alisema kuwa moja ya mpango huo ni kutoa elimu kwa jamii na wanafunzi kuona kwamba suala hilo linaongelewa kwa uwazi kuanzia ngazi ya familia kuelekea kwenye taasisi za elimu ili kila mmoja kuwa na uelewa mpana kuhusu mpango wa hedhi salama.

Profesa Makubi alisema kuwa mwongozo huo pamoja na mambo mengine utahakiki mwanaume anakuwa mshiriki mkubwa katika utekelezaji wa mpango wa hedhi salama kwa wanawake ili kuwezesha upatikanaji wa taulo za kike zenye ubora zisizoleta athari kwa watumiaji.

“Serikali tumekusudia kuweka mwongozo ambao utatuongoza sisi serikali kuanzia ngazi ya wizara na wadau wetu kuhakikisha wanawake wanakuwa na hedhi salama, kupitia wizara ya elimu na wizara ya Tawala za mikoa na serikali za mitaa kutoa elimu kupitia walimu au maafisa afya kwenda kwenye taasisi za elimu kufundisha mpango wa hedhi salama,”Alisema Profesa Makubi.

Katibu huyo Mkuu wizara ya afya amekiri kuwa kwa sasa kumekuwa na matumizi ya chini ya taulo za kike zenye ubora kwa wanawake na wanafunzi wasichana hali inayofanya hedhi salama kuwa na kiwango cha chini.

Awali Mganga Mkuu wa mkoa Kigoma,Dk.Jesca Leba alisema kuwa mkoa una asilimia 16 ya shule za msingi zinazotoa taulo za kike kwa wasichana huku ukiwa na asilimia nane ya vyoo maalum ambavyo wanafunzi wasichana wanaweza kuvitumia kwa mahitaji ya hedhi ambapo shule zenye vyumba maalum kwa huduma hiyo vikiwa ni asilimia 12.

Dk.Leba alisema kuwa hata hivyo kumekuwa na nafuu kwa shule za sekondari ambapo mkoa una jumla ya shule 80 za sekondari sawa na asilimia 37 ya shule zenye vyumba maalum kwa ajili ya kutumika kwa masuala ya hedhi salama.

“Ufinyu wa bajeti kwa taasisi zinazopaswa kuweka miundo mbinu inayohudumia hedhi salama ikiwemo miundo mbinu ya maji imekuwa changamoto kubwa katika kuhakikisha masuala ya hedhi salama yanatekelezwa kwenye shule za msingi na sekondari mkoani Kigoma,”Alisema Mganga Mkuu wa mkoa Kigoma.

Akizungumza katika maadhimisho hayo Mke wa Makamu wa Raisi wa Tanzania, Mbonimpaye Philp Mpango alisema kuwa suala la hedhi salama ni la jamii nzima na siyo wanawake peke yako hivyo wadau wote wanapaswa kuungana ili kufanikisha mpango wa hedhi salama kwa wanawake.

Alisema kuwa ni lazima kuwepo na mpango rahisi utakaowezesha kutekelezwa kwa mpango wa hedhi salama kwa wanawake na wasichana kujisitiri kwa kupata taulo zenye viwango vinavyotakiwa kwa gharama nafuu na kwa urahisi.

Mke wa Makamu wa Raisi alisema kuwa bado changamoto ni nyingi kwa wanawake na wasichana hasa uwepo wa vyoo bora, vyumba vya kubadilishia, maeneo maalum ya utupaji wa tauli zilizotumika sambamba na uelewa mdogo wa jamii na wasichana kuhusiana na elimu ya hedhi salama huku wasichana wakikabiliwa na changamoto ya uwezo mdogo wa kugharamia upatikanaji wa taulo za kike.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post