SERIKALI YAZINDUA KAMATI YA WANAWAKE YA HUDUMA JUMUISHI ZA KIFEDHA


Naibu Waziri wa Fedha na mipango Hamad Hassan Chande akiongea kwenye uzinduzi wa baraza la Taifa la huduma jumuishi za fedha (WACFI) Jijini Dodoma ambapo ameeleza kuwa azma ya Serikali ni kupunguza utofauti ulipo katika upatikanaji na utumiaji wa huduma za fedha kati ya mwanamke na mwanaume utapungua kwa zaidi ya asilimia 9
Gavana wa Benki kuu ya Tanzania Prof. Florens Luoga akiongea kwenye uzinduzi wa baraza la Taifa la huduma jumuishi za fedha (WACFI)lenye lengo la kuwainua wanawake,uzinduzi huo umefanyika leo jijini Dodoma .

 
Na Dotto Kwilasa,Malunde 1 Blog-DODOMA

SERIKALI kwa kushirikiana na sekta binafsi kupitia baraza la taifa la huduma jumuishi za fedha imezindua rasmi kamati ya wanawake ya huduma jumuishi za fedha (WACFI)yenye wajumbe 22 kutoka wizara mbalimbali za Serikali ,Taassi na Asasi  za kiraia inayolenga kuongeza idadi ya wanawake katika sekta ya fedha.

Akiongea katika uzinduzi huo,Naibu Waziri wa fedha na mipango Hamad Hassan Chande amesema hatua hiyo ni muendelezo wa utekelezaji wa mikakati ya Mpango wa Pili wa huduma Jumuishi za Fedha unaolenga kujumuisha zaidi kundi la wanawake katika matumizi ya huduma rasmi za fedha nchini. 

Amesema,suala  la kuinua wanawake kiuchumi kwa kuongeza ushiriki wao katika sekta ya fedha ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapindunzi ya mwaka 2020, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 -2025/26) na Mpango Kabambe wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa mwaka 2020/21-2029/30. 

"Kamati hii ni muhimu na ina jukumu kubwa katika kubuni, kuchochea na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mikakati inayolenga kuongeza idadi ya wanawake katika kuzifikia na kuzitumia huduma rasmi za fedha na hatimaye kunyanyua kipato cha mwanamke;

Ni matumaini yangu kuwa, baada ya uzinduzi wa leo mtahakikisha lengo la Serikali la kupunguza utofauti ulipo katika upatikanaji na utumiaji wa huduma za fedha kati ya mwanamke  na mwanaume utapungua kwa zaidi ya asilimia 90,"amesema Naibu Waziri huyo wa fedha.

Vilevile amesisitiza kuwa azma ya kumnyanyua mwanamke kiuchumi ifanyiwe kazi ipasavyo, kwa kushirikana na Kamati ya ushauri ya Kitaifa ya Utekelezaji wa ahadi za Nchi kuhusu Kizazi chenye Usawa na kuongeza kuwa  utakapofanyika  utafiti mwingine wa kisekta, baada ya utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha wa mwaka 2018-2022, idadi ya watanzania watu wazima wanaotumia huduma rasmi za fedha itakuwa imeongezeka mpaka asilimia 75 mwaka 2022.

"Ninategemea kuona mbali na kutekeleza malengo mtakayokuwa mmejiwekea kupitia Kamati hii yanayohusu masuala ya fedha, pia mtatekeleza mikakati yenye kuhamasisha wadau wa huduma za fedha kutoa elimu ya masuala ya fedha kwa wanawake hasa waishio vijijini ili waweze kunufaika na huduma na bidhaa za fedha,"amesisitiza 

Mbali na hayo ameeleza kuwa elimu ya fedha ni muhimu ili kuwaondolea hofu wanawake walio wengi katika kutumia huduma hizo ikiwemo mikopo na kwamba bado kuna umuhimu wa kuwafundisha wanawake namna ya kusimamia mikopo na kujitetea kisheria pale panapokuwa na uporaji wa fedha zao za mikopo dhidi ya wenzi wao ili wasipate changamoto yakufanya marejesho.

"Kuna umuhimu kwa wanawake kupewa elimu ya namna ya kuweka akiba, kufanya uwekezaji, kukata bima na kujiandaa na maisha ya uzeeni,ipo haja ya kuwahamasisha wadau wa sekta ya fedha kupendekeza mikakati itakayoongeza upatikanaji wa takwimu za kijinsia hasa kutoka kwa sekta binafsi ili zitusaidie  kufanya maamuzi ya kisera kwa kuzingatia usawa wa kijinsia,"amesema.

Kwa upande wake Gavana wa Benki ya Tanzania,Prof. Florens Luoga amesema  Tanzania imekuwa ikitekeleza Mpango wa Pili wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha (2018-2022), ambao unalenga kuongeza idadi ya watu wanaotumia huduma rasmi za fedha kutoka asilimia 65 mwaka 2017 hadi asilimia 75 mwaka 2022. 

Amesema Mpango huo unatekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi kupitia Baraza la Taifa la Huduma Jumuishi za Fedha, ambalo lina wajumbe 22, kutoka Wizara mbalimbali za Serikali, taasisi na asasi zisizo za Serikali.

"Mpango huu wa Taifa unasisitiza kuongeza idadi ya wanawake inayofikiwa na kutumia huduma rasmi za fedha, umeelekeza, kuundwa kwa Kamati ya Wanawake ili kuratibu shughuli zote zinazohusu wanawake nchini katika Sekta ya Fedha pamoja na kushauri njia bora ya kutatua changamoto zinazowakumba wanawake katika kufikia na kutumia huduma rasmi za fedha,"amesema.
 
Ametaja lengo la mpango huo kuwa ni kuhakikisha idadi kubwa ya wanawake wanaofikiwa na kutumia huduma rasmi za fedha inaongezeka, kutoka asilimia 61 mwaka 2017 hadi asilimia 73 mwaka 2022, pia kupunguza pengo la uwiano wa kijinsia katika utumiaji wa huduma rasmi za fedha kati ya wanawake na wanaume kwa asilimia 90. 

"Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, wanawake ni asilimia 51.3 ya watu wote nchini na asilimia 54 ya watu wenye umri wa miaka 60 na zaidi na asilimia 53.3 ya wafanyakazi wote wanaojishughulisha na kilimo au biashara zisizo rasmi ni wanawake pia  katika biashara, asilimia 54 ya wamiliki wa biashara ndogo ndogo, na za kati (MSMEs) nchini ni wanawake,

"Kwa upande wa elimu, asilimia sita ya wanawake zaidi ya wanaume hawana elimu rasmi, huku asilimia 67 ya wanawake dhidi ya asilimia 78 ya wanaume ndiyo wanajua kusoma na kuandika lugha ya Kiswahili na   kwa  upande wa lugha ya kiingereza ni asilimia 22 ya wanawake ikilinganishwa na asilimia 31 ya wanaume ndio wanajua kusoma na kuandika,"ameeleza Gavana Luoga.

Amesema kwa kuzingatia takwimu hizo ni wazi kuwa wanawake wanakabiliwa na changamoto kubwa katika kupata huduma za fedha na hii ni kutokana na kutokuwa na elimu ya kutosha katika masuala ya fedha, mtazamo hasi kwa baadhi ya jamii kuhusu wanawake pamoja na uwepo wa mila na tamaduni potofu zinazosababisha mwanamke kutozifikia huduma rasmi za fedha. 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post