AFISA AFYA AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA MAKOSA YA RUSHWA NA UHUJUMU UCHUMI

 


Mshitakiwa Simon Nyandwera


Na Dinna Maningo,Tarime

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilaya ya Tarime mkoa wa Mara imemfikisha Mahakamani aliyekuwa Afisa Afya wa halmashauri ya Mji wa Tarime, Simon Nyandwera akikabiliwa na mashtaka matano yakiwemo ya kuisababishia hasara Serikali,kugushi nyaraka,ufujaji na ubadhilifu.


Mshitakiwa huyo amepandishwa kizimbani Aprili,19,2022 nakufunguliwa shauri la Uhujumu Uchumi namba 13 la mwaka 2022.


Mbele ya Hakimu mkazi Mwandamizi wa mahakama ya wilaya ya Tarime Yohana Myombo,Mwendesha mashtaka wa TAKUKURU na Wakili wa Serikali Mwinyi Yahaya akisoma mashtaka matano,alisema shtaka la kwanza ni kugushi kinyume na vifungu vya 333,335 (a) na 337 vya kanuni ya adhabu  Sura ya 16 mapitio ya 2022.


Wakili Yahaya ameieleza mahakama kwamba Octoba 17,2014 katika halmashauri ya Mji wa Tarime,kwa lengo la kudanganya,mshitakiwa alitengeneza nyaraka ya uongo ambayo ni Delivery Note namba 0325 ya tarehe 17/10/2014,kuonyesha kwamba ilikuwa imetolewa na RODDEO GARAGE baada yakufanya ukaguzi wa gari la Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa ajili ya kulifanyia matengenezo,jambo alilojua si kweli.


Shtaka la pili alisema ni la kugushi kinyume cha vifungu hivyo vya kanuni ya adhabu ,Yahaya aliieleza mahakama kuwa Octoba 17,2014 katika halmashauri hiyo kwa lengo la kudanganya,mshitakiwa alitengeneza nyaraka ya uongo ambayo ni Profoma/Invoice namba 00083 ya tarehe 17,10,2014 yenye thamani ya sh.Milioni 4,125,000,kuonyesha kwamba ilikuwa imetolewa na RODDEO GARAGE baada ya kulifanyia matengenezo gari la Halmashauri hiyo jambo alilojua kuwa si kweli.


Yahaya alisema kuwa shtaka la tatu ni kugushi kinyume na vifungu hivyo vya kanuni ya adhabu kwamba Oktoba 17,10,2014 katika halmashauri hiyo kwa lengo la kudanganya,mshitakiwa alitengeneza nyaraka ya uongo ambayo ni stakabadhi namba 93 ya tarehe 17,10,2014,yenye thamani ya sh.Milioni 4,125,000,kuonyesha kwamba ilikuwa imetolewa na RODDEO GARAGE baada ya kulifanyia matengenezo gari la Halmashauri hiyo jambo alilojua siyo kweli.


Shtaka la nne ni Ufujaji na Ubadhilifu kinyume na kifungu cha 28 (1) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa Sura ya 329 mapitio ya 2002.Wakili Yahaya ameieleza mahakama kwamba Octoba 17,2014 katika ofisi za halmashauri ya Mji wa Tarime,kwakukosa uaminifu mshitakiwa alibadilisha matumizi ya sh.Milioni 4,125,000 kwa ajili ya matumizi binafsi fedha alizokuwa amekabidhiwa na halmashauri hiyo kwa ajili ya matengenezo ya gari la Halmashauri hiyo.


Yahaya aliongeza kuwa shtaka la tano ni kuisababishia hasara Serikali kinyume na aya ya 10 (1) ya Jedwari la kwanza pamoja na vifungu vya 57,(1) na 60 (2) vya sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 mapitio ya 2019.Wakili huyo ameieleza mahakama kwamba Oktoba, 17,2014 katika ofisi za halmashauri hiyo,mshitakiwa akiwa mtumishi wa halmashauri kwa vitendo vyake vya maksudi,aliisababishia halmashauri hiyo hasara ya sh.Milioni 4,125,000.


Mshitakiwa amekana mashtaka yote yanayomkabili na ameshindwa kutimiza masharti ya dhamana hivyo kupelekwa mahabusu katika gereza la wilaya ya Tarime na kesi yake itatajwa Mei,2,2022 kwa ajili ya kusikilizwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments