MAAFISA USTAWI WA ARUSHA DC WATOA MSAADA KWA WATU WENYE UHITAJI - MALUNDE 1 BLOG | Fahari ya Shinyanga

Breaking

Tuesday, April 12, 2022

MAAFISA USTAWI WA ARUSHA DC WATOA MSAADA KWA WATU WENYE UHITAJI


Na Rose Jackson, Arusha

Katika kuadhimisha siku ya Ustawi wa Jamii Duniani, wataalamu wa Kitengo cha Ustawi wa Jamii wa halmashauri ya Arusha, wameadhimisha siku hiyo muhimu kwa kutoa msaada kwa watu wenye mahitaji maalum, kata ya Oldonyowas, wilaya ya Arumeru.

Akizungumza wakati akikabidhi msaada huo Afisa Ustawi wa Jamii halmashauri ya Arusha Neema Mwina, amesema kuwa, katika kuadhimisha siku hiyo muhimu kwao, wamewiwa kutoa msaada wa chakula na nguo kwa watu wenye ulemavu, watoto waishio katika mazingira hatarishi pamoja na wazee, lengo likiwa ni kutatua changamoto zinazowakabili watu hao, katika nyanja za kiuchum na kijamii.

"Tunatambua changamoto zinazowakabili jamii, hasa makundi maalumu ya wenye uhitaji, leo tumeamua kuadhimisha siku yetu kwa kutoa kidogo tulichonacho kama ishara ya upendo na kuwathamini wahitaji", amefafanua Neema.

Aidha, Afisa Utawi Neema ameutaja msaada uliotelewa ni kilo 300 za mchele, mifuko 4 ya sabuni ya unga, viroba 7 vya nguo, pamoja na katoni moja ya minara ya sabuni, msaada uliotolewa kwa watu 30, kutoka katika vijiji vinne vya kata ya Oldonyowas.

Hata hivyo wananchi hao waliopata msaada, wameshukuru halmashauri kwa kuwakumbuka watu wenye uhitaji, na kukikiri kuwa wanakabiliwa na hali ngumu ya kimaisha, huku wakitoa wito kwa serikali kuendelea kuwawezesha watu wa wenye uhitaji hata kwa kuwapa mitaji ya kufanya biashara ndogo ndogo.

"Napenda kuwashukuru sana kwa huduma hii mliyotuletea, tumefurahi sana kwasababu tuko katika hali ngumu ya kimaisha, tuna watoto wanaotutegemea wengine ni wajane na wengine ni yatima, tuna mzigo mzito sana katika maisha",alisema Martha Mollel mmoja wa waliopokea msaada huo.

Naye mmoja wa wadau walioshiriki katika kutoa msaada huo Yohana Msomba amesema imekuwa ni desturi yao kuitembelea jamii ya watu wenye uhitaji hususani watoto yatima na wale wanaioshi katika mazingira hatarishi, ili kuwasaidia kutatua changamoto zinazowakabili na kuitaka jamii kuonyesha upendo kwao badala ya kuwabagua.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

No comments:

Post a Comment

Pages