WANANCHI KARAGWE WAISHUKURU TAASISI YA MANAGEMENT AND DEVELOPMENT FOR HEALTH (MDH) KUFANYA KLINIKI TEMBEZI YA KIFUA KIKUU

Gari la Kliniki tembezi pamoja na baadhi ya madaktari na wakwanza kulia ni Mratibu wa Kifua kikuu na Ukoma Wilaya ya Karagwe Dkt. Misango Maxmillian
AMratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma Wilaya ya Karagwe Dkt. Misango Maxmillian akitoa Elimu ya dalili za Kifua Kikuu kwa wananchi
Wananchi wakiorodheshwa kwenye kitabu cha kumbukumbu
Wananchi wa Wilaya ya Karagwe wakisubiri kuingia ndani ya gari la Kliniki tembezi kupata Huduma ya vipomo vya TB
Baadhi ya watu waliopata vipimo na kugundulika na ugonjwa wa kifua kikuu na kuanzishiwa matibabu


Na Mbuke Shilagi Kagera.

Wanannchi wa Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera wameishukuru Taasisi ya Management and Development for Health (MDH) kwa  kufanya kliniki tembezi ya kifua kikuu (TB) wilayani humo.

Akizungumza na Malunde 1 Blog mmoja wa wananchi hao Aporinary Zamunuga amesema kuwa huduma ya kliniki tembezi imewasaidia kupata vipimo vya TB na tiba bila malipo.

Bw. Zamunuga ameongeza kuwa amepokea matibabu katika gari la kliniki tembezi na kugundulika kuwa na ugonjwa wa kifua kikuu na kuanzishiwa dozi.

"Nilianza kuona dalili za kifua kikuu kwa muda wa miezi sita iliyopita,  baada ya kufika huduma hiyo ya kliniki tembezi tayari nimepata vipimo na kuanza tiba bila kulipia chochote, nawashukuru sana MDH kwa huduma hii" ,amesema.

Amewaasa wananchi wenzake kujitokeza pale wanaposikia imetangazwa kuwepo kwa huduma hiyo ya kiliniki tembezi katika maeneo yao, ili kupimwa na kutambua afya zao na kupata tiba haraka kwa wale watakaobainika  kuwa na ugonjwa huo.

Kwa upande wake Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma Wilaya ya Karagwe Dkt. Misango Maxmillian amesema kuwa Kliniki tembezi inasaidia wananchi ambao hawawezi kufika hospitali na wasio kuwa na fedha, ambao hupata vipimo na matibabu bure.

"Huduma zake ni rahisi na zinafikika, na pia zinasaidia wananchi ambao hawana uwezo wa kufika hospitali na wasio na gharama za kupata vipimo", amesema.

Dkt. Maximilian amesema kuwa wananchi wanapopimwa na kugundulika na ugonjwa wa kifua kikuu, wanaanzishiwa tiba wakati huo huo na kwamba kwa Wilaya ya Karagwe tayari wapo wagonjwa 130 kwa kipindi cha mwezi Januari mpaka Machi mwaka huu, ikiwa idadi kubwa ni wenye umri wa miaka 45 kupanda juu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post