MTOTO HUYU ANASUMBULIWA NA SARATANI YA MACHO...MSAADA WA MATIBABU UNAHITAJIKA


Agatha Bulunja akiwa na mtoto wake Janety Betho, ambaye anasumbuliwa na saratani ya macho akiomba msaada wa matibabu kwa wasamaria wema. Wasiliana na Mama huyu kwa simu namba 0758267338
Muonekano wa Mtoto Janety Betho kabla ya kuugua saratani ya macho

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

MWANAMKE Agatha Bulunja (30) mkazi wa Ndala Manispaa ya Shinyanga mkoani Shinyanga, anaomba msaada wa matibabu ya mtoto wake Jenety Betho (4), ambaye anasumbuliwa na tatizo la saratani ya macho iliyosababisha apoteze uwezo wa kuona tena.

Ameomba msaada huo leo wakati akizungumza na vyombo vya habari nyumbani kwake, kuwa mtoto wake huyo hali yake inazidi kuwa mbaya na hana fedha za kumpatia matibabu ya kufanyiwa upasuaji.

Amesema alimzaa mtoto huyo mwaka 2018 akiwa mzima kabisa na macho yake yote yanaona, lakini alivyofikisha miezi saba ndipo tatizo la kuugua Saratani ya macho likaanza.

“Mtoto huyu nilianza kumpatia matibabu katika Hospitali ya Rufaa mkoani Shinyanga, na baadaYe tukapewa Rufaa ya kwenda Muhimbili ndipo nikaambiwa anatakiwa afanyiwe upasuaji, lakini kutokana na kutokuwa na uwezo ikabidi nirudi nyumbani,”amesema Bulunja.

Aidha amesema Januari mwaka huu 2022 hali ya mtoto huyo ndipo ikabadilika na kuwa mbaya zaidi, pamoja na kuota nyama kwenye macho na kuyaziba na kuacha kuona kabisa, huku akilia usiku kucha kwa kuugulia maumivu na kumpatia dawa za kutuliza maumivu hayo.

Amesema kutokana na hali ya mtoto wake kuendelea kuwa mbaya zaidi, anawaomba wasamaria wema wamsaidie ili mtoto wake apate matibabu na kurudi katika hali yake ya kawaida kama zamani.

Kwa upande wake mama mwenye nyumba ambayo amepanga mwanamke huyo, Efania Kelvin, amesema wamekuwa wakimpatia msaada wa mahitaji muhimu ikiwemo chakula kwa sababu hana kazi ya kumuingizia kipato kutokana na kubaki kumuuguza mwanaye hapo nyumbani bila ya mafanikio.

Amesema kutokana na hatua ya Saratani ambayo amefikia mtoto huyo, ana hitaji kupatiwa matibabu katika hospitali kubwa, na kutoa wito kwa wadau ambao wataguswa na mtoto huyo wamsaidie ili apate matibabu.

Kwa mtu yoyote atakayeguswa na habari na kuamua kumsaidia Mwanamke huyo awasiliane naye kwa simu namba 0758267338

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments