WASANII WASHINDI WA TUZO ZA MUZIKI TANZANIA WAPATA ELIMU NA KUJIUNGA NA NSSF


Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa NSSF, Lulu Mengele, akitoa mada kuhusu umuhimu wa kujiwekea akiba kwa baadhi ya wasanii walioshinda Tuzo za Tanzania Music Award. Ambapo Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ilitoa zawadi mbalimbali kwa wasanii walioshinda ikiwepo zawadi ya kuwachangia NSSF na NHIF katika kipindi cha mwaka mmoja na baada ya hapo wasanii wenyewe wataendelea kuchangia.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA), Matiko Mniko, akitoa neno la utangulizi wakati wa Semina ya kuwajengea uelewa baadhi ya wasanii washindi wa Tuzo za Muziki Tanzania kuhusu elimu ya Hifadhi ya Jamii kwa upande wa NSSF na Bima ya Afya (NHIF).
Afisa Matekelezo Mkuu wa Sekta Isiyo Rasmi, Abdulaziz Abeid akitoa mada kwa baadhi ya wasanii washindi wa Tuzo za Muziki Tanzania kuhusu umuhimu wa kujiunga, kuchangia ili wajiwekea akiba kwa maisha yao ya sasa na baadaye.
Msanii wa Muziki, Snura Mushi ambaye ni mmoja wa mshindi kwenye Tuzo za Muziki Tanzania akiuliza maswali mbalimbali kuhusu NSSF mara baada ya mada zilizotolewa na NSSF kwenye Semina ya kuwaongezea uelewa wa Hifadhi ya Jamii iliyoandaliwa na BASATA.
Baadhi ya maofisa wa NSSF wakijibu maswali mbalimbali kutoka kwa baadhi ya wasani walioshinda Tuzo za Muziki Tanzania mara baada ya kupata elimu ya Hifadhi ya Jamii ili waweze kujiunga na kujiwekea akiba kwa maisha yao ya sasa na baadaye.
Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa NSSF, Lulu Mengele akifuatilia jinsi wasani Snura Mushi na Sholo Mwamba wakijaza fomu za kujiunga na NSSF, ambapo mwaka huu katika Tuzo za Wanamuziki Bora wasanii hao walikuwa miongoni mwa wasanii bora
Baadhi ya Wafanyakazi wa NSSF wakiwasaidia wasanii kujaza fomu za kujiunga na NSSF ambapo Wizara itawalipia michango ya mwaka mmoja na baada ya hapo wasanii hao wataendelea kuchangia wenyewe


***
Na Mwandishi wetu 

Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umetoa elimu ya Hifadhi ya Jamii kwa baadhi ya wasanii ambao ni washindi wa Tuzo za Muziki Tanzania kuhusu umuhimu wa kujiunga na kujiwekea akiba kwa maisha yao ya sasa na baadaye.


Baada ya elimu hiyo wasanii hao walipata fursa ya kujiunga na NSSF ikiwa ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia kwa Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Mohamed Mchengerwa ambaye aliahidi kuwa Wizara pamoja na kutoa zawadi kwa wasanii walioshinda vilevile Wizara iliona ni vema kuwalipia NSSF wasanii hao ambao wameshinda kwa kipindi cha mwaka mmoja na baadaye wataendelea wenyewe.


Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa NSSF, Lulu Mengele alieleza umuhimu wa wasanii kujiunga, kuchangia ili wajiweke akiba kwa maisha yao ya sasa baadaye ambapo pindi watakapokosa kipato waweze kunufaika na mafao mbalimbali ikiwemo pensheni ya uzee.


Naye, Abdulaziz Abeid ambaye ni Afisa Matekekezo Mkuu wa Sekta Isiyo Rasmi alisema Mfuko umeweka mifumo rahisi na rafiki kwa kila Mtanzania aliyejiajiri mwenyewe kujiwekea akiba. Hivyo alitoa wito kwa wasanii kuchangamkia fursa hiyo.


Kwa upande wake, Mratibu wa Tuzo za Muziki kutoka BASATA, Mrisho Mrisho, aliwataka wasanii kujiunga na NSSF kwa ajili ya kujiwekea akiba ya maisha ya baadaye kwani kuna faida nyingi ambazo watanufaika nazo.


Msanii wa muziki wa singeli, ambaye alichukua Tuzo ya Mwanamuziki bora wa Singeli kwa wasanii wanawake, Snura Mushi, aliishukuru NSSF kwa kuwafikia wasanii ili waweze kujiunga na kujiwekea akiba kwa maisha yao ya sasa na baadaye.


Naye, mkali wa singeli, Sholo Mwamba aliipongeza NSSF kwa kuwafikia wasanii na kuwaomba wasanii wengine ambao hawajashinda kuchangamkia fursa hiyo ya kujiunga na NSSF kwani ni Mfuko wenye faida kubwa sana.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments