'HOUSE BOY' AMUUA 'HOUSE GIRL'...AJARIBU KUJIUA YASHINDIKANAKIJANA ambaye alikuwa mfanyakazi wa kulisha ng'ombe amemuua msichana wa kazi za ndani kwenye nyumba waliyokuwa wakifanya kazi pamoja huku chanzo kikiwa bado hakijafahamika.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, ACP Pius Lutumo amesema kuwa, mtuhumiwa na marehemu walikuwa wakifanya kazi kwa mtu aliyefahamika kwa jina moja la Samwel.


Amesema kuwa, mtuhumiwa ambaye jina limehifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi umri wa miaka 27 alimuua Dawiya Mshihiri (30) kwa kumshambulia na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili.


"Mtuhumiwa baada ya tukio hilo alijaribu kujiua kwa kunywa sumu, lakini hakufanikiwa na kukamatwa na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Tumbi kwa matibabu akiwa chini ya ulinzi wa polisi,"amesema Lutumo.


Aidha, amesema kuwa mtuhumiwa na marehemu walikuwa wakifanya kazi kwenye nyumba moja na Polisi wanaendelea na uchunguzi juu ya tukio hilo.


Amebainisha kuwa, mara upelelezi utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria na anawasihi wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi.

CHANZO - DIRA MAKINI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post