WAFAMASIA WATOA TAMKO ZITO WATOA HUDUMA WASIO NA TAALUMA YA DAWA KUHUDUMIA KWENYE MADUKA YA DAWA


Mfamasia na Katibu Mkuu wa Chama cha Wafamasia Tanzania, Benson Katundu katika mkutano wake na waandishi wa habari Mjini Shinyanga leo Ijumaa Aprili 22,2022 kwa ajili kukemea ukiukwaji wa sheria inayosimamia maduka ya dawa muhimu.
Mfamasia na Katibu Mkuu wa Chama cha Wafamasia Tanzania, Benson Katundu katika mkutano wake na waandishi wa habari Mjini Shinyanga leo Ijumaa Aprili 22,2022 kwa ajili kukemea ukiukwaji wa sheria inayosimamia maduka ya dawa muhimu


Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Kufuatia kusambaa kwa video kadhaa mitandaoni zikionesha watoa huduma wasio na taaluma ya dawa wakihudumia katika maduka ya dawa kinyume na miongozo sheria na taratibu zinazoongoza biashara ya maduka ya dawa muhimu nchini, Chama cha Wafamasia Tanzania (Phamarceutical Society of Tanzania PST), kimekemea na kulaani vikali vitendo hivyo kwani ni hujuma kwa afya za Watanzania.


Akizungumza kwenye mkutano wake na Waandishi wa Habari Mjini Shinyanga leo Ijumaa Aprili 22,2022, Mfamasia na Katibu Mkuu wa Chama cha Wafamasia Tanzania, Benson Katundu amesema wanalaani vitendo vya watoa huduma katika maduka ya dawa au wamiliki wa maduka ya dawa kuajiri watoa huduma wasio na taaluma ya dawa kutoa huduma hizo jambo ambalo ni hatari kwa afya za Watanzania.


Amesema watoa huduma katika maduka mengi wameonekana wakifanya vitendo visivyokubalika katika maduka hayo ikiwemo, uchomaji wa sindano za uzazi wa mpango, kufanya vipimo vya magonjwa mbalimbali kwenye maduka kinyume na utaratibu, uzalishaji wajawazito katika maduka ya dawa na kufanya matibabu yasiyoruhusiwa katika maduka hayo.


Kitundu ameongeza kuwa pia kuna uuzwaji holela wa dawa za moto (antibiotics) zisizoruhusiwa kuuzwa katika maduka hayo ya dawa muhimu ambazo zina athari ikiwemo kusababisha usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa, kusababisha ulemavu na hata kusababisha vifo.


“Tunakemea na kulaani vitendo hivi kwani dawa ni sumu ambazo zinaweza kuleta ulemavu wa kudumu ama kupoteza maisha endapo hazitatumiwa kwa usahihi”,amesema Kitundu.


Katibu Mkuu huyo wa PST amesema wanaliomba Baraza la Famasi kuangalia upya mifumo yake ya ukaguzi wa maduka ya dawa muhimu yaliyoko mijini na vijijini kubaini uhalali wake ili kupunguza vitendo hivi vya ukiukwaji wa taratibu za utoaji huduma katika maduka hayo, jambo ambalo linazuia baadhi ya watu kutopata huduma za afya katika vituo vilivyoidhinishwa kisheria.


“Lengo la uanzishwaji wa maduka ya dawa muhimu ((DLDM) lilikuwa ni kusogeza huduma za dawa kwa wananchi waishio maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji .Tumeendelea kushuhudia utitiri wa maduka ya dawa muhimu yakiendelea kufunguliwa maeneo ya mijini pasipo kufuata utaratibu uliowekwa”,ameongeza Kitundu.


Amebainisha kuwa kada ya ufamasia imegawanyika katika ngazi kuu tatu ambazo ni Wateknolojia dawa wasaidizi wanaosoma kwa miaka miwili 2, Wateknolojia dawa wanaosoma kwa miaka mitatu na Wafamasia wanaosoma kwa miaka minne na kufanya internship kwa mwaka mmoja


 Amesema wataalamu wote hao hutakiwa kufanya mtihani maalumu wa kusajiliwa na baraza la Famasi Tanzania ili kuweza kupatiwa leseni za kutekeleza majukumu yao katika maeneo mbalimbali.


Amesema upo ushahidi wa watoa huduma wengi waliopata mafunzo ya utoaji dawa (Accredited Drug Dispensing Outlet- ADDO) wakitekeleza majukumu mengine nje ya uuzaji wa maduka ya dawa huku wakiajiri watu wasio na taaluma ya uuzazi dawa za binadamu katika maduka yao.


“Chama cha Wafamasia Tanzania kinaliomba Baraza La Famasi Tanzania Kutathimini upya kama kuna haja na hitaji la kuendelea kutoa mafunzo ya (ADDO) ilhali wataalam wa dawa wenye mafunzo ya miaka miwili na miaka mitatu na miaka mitano wakiendelea kuzalishwa kutoka vyuo vya kati vya afya 218 vikiwemo vya serikali na binafsi, na vyuo vikuu vya afya vinne vilivyopo nchini”,amesema Kitundu.

“Hakuna kada ya afya inayotoa mafunzo ya mwezi mmoja na watu hao kuingia kuwahudumia watanzania, hivyo Chama cha Wafamasia tunaomba mafunzo haya ya ADDO kusitishwa kwani afya ya mwanadamu haijaribiwi tuwape wataalamu nafasi ya kutekeleza majukumu yao kwa ustawi wa taifa letu”,ameeleza.


Katika hatua nyingine uongozi wa Chama cha Wafamasia Tanzania unawaelekeza wafamasia wa mikoa na wafamasia wa Halmashauri kuongeza weledi katika kusimamia kwa umakini mkubwa uanzishwaji wa maduka ya dawa muhimu katika maeneo yao na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa maduka hayo ili kuhakikisha maduka ya dawa muhimu yanahudumiwa na wataalamu wenye sifa za kutoa huduma za dawa kwa wananchi.


“Uongozi wa Chama cha Wafamasia tunaendelea kuwasisitiza wataalamu wa dawa wote nchini kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kufuata miongozo taratibu na kanuni za taaluma bila kuvunja sheria ya nchi kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa watanzania.

Aidha chama hakitamfumbia macho mtaalamu yeyote atakayethibitika pasina shaka kukiuka misingi na maadili ya taaluma hii adhimu ya ufamasia atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria na tuwaomba wananchi kuwafichua watu wasio na sifa ya kutoa huduma katika maduka ya dawa”,amesema Kitundu.


Katundu ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwawateua wafamasia Bi. Rosemary William Slaa kuwa Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa Bohari ya dawa (MSD) na Mfamasia Mavere Tukai kuwa Mtendaji mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) akibainisha kuwa ni imani ya PST kuwa wataongeza ufanisi katika chombo hicho.


“Pia tunaipongeza serikali kutoa nafasi za ajira hususan katika sekta ya afya kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika vituo vya kutolea huduma za afya. Chama kinaziomba wizara zinazohusika katika ajira hizo kutoa kipaumbele pia kwa kuajiri wataalam wa dawa wengi ili kuweza kuongeza ufanisi wa huduma za kifamasia katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini kwa kuhakikisha dawa bora na vifaa tiba bora vinapatikana kwa kufanya maoteo sahihi kama wataalam wa dawa ili kuhakikisha matibabu sahihi yanatolewa kwa wagonjwa”,amesema Kitundu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post