WATENDAJI WALIOIBA SUMU KIKAANGONI


Balozi wa zao la pamba Aggrey Mwanri akitoa maelekezo kwa wakulima Iparamasa
Dawa zilizokamatwa kwa wakala wa duka la pembejeo Iparamasa.

Na Daniel Limbe, Chato

SERIKALI imetoa siku saba kurejeshwa sumu za wakulima wa zao la pamba zinazodaiwa kuibwa na baadhi ya watendaji wa vyama vya ushirika wa mazao (Amcos) wilayani Chato mkoani Geita.


Hatua hiyo inafuatia kukamatwa chupa 104 za sumu aina ya ekapaki kwenye duka la wakala wa uuzaji wa pembejeo za kilimo kwenye kata ya Iparamasa wilayani humo,hali inayodaiwa kudhoofisha jitihada za serikali kuinua uchumi kwa wakulima.


Kauli hiyo imetolewa leo na Balozi mteule wa zao la pamba nchini, Aggrey Mwanri, wakati akikagua na kuzungumza na wakulima wa zao hilo kwa lengo la kuendelea kuhamasisha kilimo chenye kuzingatia kanuni bora kwa manufaa ya kaya na taifa kwa ujumla.


Hata hivyo balozi huyo, ameagiza kukamatwa na kufikishwa mahakamani, Katibu wa chama cha ushirika wa mazao kata ya Iparamasa (hakumtaja jina) kutokana na tuhuma za kuiba sumu zilizotolewa na serikali kwaajili ya kuwagawia wakulima ili kutokomeza wadudu washambuliao zao la pamba.


Amesema serikali kupitia bodi ya pamba nchini (TCB) iliwakasimisha viongozi wa Amcos jukumu la kuwagawia sumu hizo wakulima ili kurahisha huduma, lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida baadhi ya viongozi hao wamekuwa wakiwauzia wafugaji wa ng'ombe kwaajili ya kuogesha mifugo yao kinyume na kusudio la serikali.


Kutokana na hali hiyo, akalazimika kuagiza kurejeshwa kwa sumu zote zilizotolewa kinyume cha utaratibu ndani ya siku 7 na kwamba iwapo kuna mtu yoyote ambaye aliuziwa sumu hizo wakati siyo mkulima wa zao la pamba anatakiwa kujisalimisha kabla hatua kali za kisheria hazijachukuliwa.


Mwanri,amedai serikali haitomfumbia macho mtu yoyote mwenye nia ovu ya kudhoofisha jitihada kubwa za serikali zilizolenga kufufua zao la pamba nchini, kutokana na zao hilo kutoa ajira nyingi kwa vijana.


Kwa upande wake mwakilishi wa Bodi ya pamba Wilayani Chato,Samwel Mdidi, amesema kwa kipindi cha msimu wa kilimo 2022/23 serikali kupitia bodi ya pamba nchini inatarajia kukusanya tani 35,000 za pamba ghafi kutoka kwa wakulima.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments