WAKUU WA MIKOA WATAKIWA KUJIFUNZA KWA MTAKA UJENZI WA SOKO LA MACHINGA


Baadhi ya Wakuu wa mikoa,makatibu tawala na Wakurugenzi wakiongozwa na Waziri wa TAMISEMI Innocent Bashungwa kukagua ujenzi wa mradi wa soko la Machinga Dodoma unaotarajiwa kukamilika Mwezi Mei mwaka huu.
Waziri wa TAMISEMI Innocent Bashungwa akiongea na waandishi wa Habari mara baada ya kukagua ujenzi wa soko la machinga Dodoma,mradi ambao amesema utarudisha hadhi ya machinga Nchini.
Msanifu mshauri wa mradi wa soko la machinga Dodoma Dkt. Ibrahim Msuya akimuelekeza jambo Waziri Bashungwa katika eneo unapojengwa mradi wa soko hilo na kueleza kuwa linatarajia kubeba zaidi ya machinga 3000 mara litakapokamilika huku likiwa na vizimba vya aina 90 vitakavyotumika kwa biashara tofauti tofauti.

Na Dotto Kwilasa, Malunde1 Blog-DODOMA.

SERIKALI imesema inatambua Sekta ya Machinga kuwa ni rasmi kutokana na mchango wake katika kuinua uchumi nchini hivyo kuwataka Wakuu wa mikoa kote nchini kuona haja ya kuboresha mazingira yao ili kurudisha heshima ya wamachinga.

Hayo yameelezwa leo Jijini hapa na Waziri wa TAMISEMI Innocent Bashungwa katika ziara yake na wakuu wa mikoa ya kujifunza kwenye mradi wa ujenzi wa soko la Machinga -Open Market, unaotekelezwa na jiji la Dodoma na kuwataka wakuu wa halmashauri zenye hadhi ya Majiji kutumia mbinu inayotumika katika ujenzi wa Soko hilo (Machinga Complex)kuwapanga wachinga kulingana na Mazingira ya maeneo yao.

Akizungumza na viongozi hao, Bashungwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametambua sekta ya machinga kuwa rasmi hivyo kwa sasa wanaenda na maono yake ya kuhakikisha wanajengewa mazingira rafiki kwa kazi zao ikiwa ni pamoja na kutekelezwa bila kuwepo kwa kikwazo chochote.

“Lengo la ziara hii ni kujifunza na wao waende kutekeleza kitu kama hiki katika maeneo yao kwani katika eneo hili tunakwenda kuwa na kitu cha kipekee ambacho hakijawahi kuwepo nchini mwetu”, amesema na kuongeza;

Mwanzoni kabisa changamoto ya machinga haikuwa na suluhu kwa sababu tuliyokuwa tunatafanya kuzitatua hayakuwa na uhalisia, hivyo kwa soko letu hapa baada ya maelekezo ya Rais kuwajengea mazingira rafiki tukaamua kutokwenda nje ya nchi kuiga wenzetu wanavyofana tukathamini vya ndani kwa kwenda eneo la Mnadani Msalato jijini hapa ili kuona ni namna gani watafanya biashara zao,

Napongeza sana ubunifu uliofanya Mtaka kwenye soko hili,hii ni fursa kwa viongozi wengine wa mikoa yenye hadhi ya majiji kama Tanga, Arusha, Mwanza, Mbeya kujifunza kwa gharama ndogo hapa hapa nchini,” amesema Bashungwa.

"Ingewezekana kwenda nje ya nchi kubuni kitu ambacho tunaweza kujifunza sisi wenyewe hivyo tunajivunia suala hili na wakuu wa mikoa, makatibu Tawala na wakurugenzi nimewaomba mje hapa ili kutafsiri kwa vitendo kwenye ngazi za mikoa maana yapo mambo makubwa tunaweza kufanya, hivyo tumieni matamko ya viongozi na maono yao kufanya haya”,amesema

Aidha, alisema kutokana na Rais Samia kutambua wamachinga kuwa ni sekta rasmi wakuu wa mikoa wanatakiwa kutekeleza agizo la kuwapanga kwa amani na utulivu.

“Badala ya kwenda nje kujifunza lakini sasa tumepata eneo ambalo wakuu wa mikoa watalitumia kujifunza katika utekelezaji wa maagizo ya Rais lakini na sisi viongozi wa mikoa lazima tuweze kusubutu na kuwa wabunidfu katika kutengeneza miradi ambayo itakuwa na tija kwa wamachinga na taifa kwa ujumla”, alisema

Bashungwa, aliongeza katika kutekeleza miradi ya kuwapanga wamachinga Rais alitoa kiasi cha Sh.bilioni 5 na kiasi cha Sh.milioni 500 kimepelekwa katika kuongezea nguvu kwenye mradi wa Machinga Open Market Dodoma.

Hata hivyo, aliupongeza uongozi wa jiji la Dodoma ukiongozwa na mkuu wa mkoa huo Antony Mtaka kwa kubuni mradi huo na kuusimamia kwa kutumia mapato yao ya ndani.

Mkuu wa mkoa wa Mbeya Juma Homela, alishukuru kwa ziara hiyo na kuahidi kwenda kufanya marekebisho ya kuboresha miradi ambayo tayari walishaianza katika maeneo yao.

“Mheshimiwa Waziri kwa niaba ya wakuu wenzangu wa mikoa tunashukuru sana kwa ziara hii ya kujifunza na tunaahidi kwenda kuifanyia maboresho miradi yetu ili kupata kitu bora kwa ajili ya wamachinga katika maeneo yetu”, alisema.

Kutokana na hayo Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe aliwataka wamachinga kuboresha biashara zao ili ziendane na hadhi ya soko hilo la kisasa huku akiwataka kukua kiuchumi Kwa kuhitimu kutoka ngazi ya chini na kwenda juu.

Kwa upande wake, Msanifu mshauri wa mradi huo, Dkt. Ibrahim Msuya amesema  soko hilo litaweza  kubeba machinga 3000 na vizimba vya aina 90 za biashara tofauti tofauti na kwamba kwa sasa wanasajili wa machinga kwa mfumo wa kidigitali kutokana na kujitokeza kwa changamoto ya baadhi kujisajili mara mbili jambo ambalo lilileta taswira mbaya.

Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa mikoa waliotembelea mradi huo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera amesema wamejifunza kupitia mradi huo na kuahidi kuwa kwenye maeneo yao watazingatia  kuwawekea mazingira rafiki machinga Ili kuwapa ufanisi wa k├ázi yao.

"Kipekee tunawashukuru wenzetu wa Dodoma sisi tumejifunza na tunaenda kuwajibika,wenzetu wako makini kwa uthubutu,tunaenda kutekeleza maelekezo tuliyoyapata,"amesisitiza Mkuu huyo wa mkoa wa Mbeya.

Wakuu hao wa mikoa waliofanya ziara ya kujifunza kuhusu mradi wa ujenzi wa soko la Machinga -Open Market, unaotekelezwa na jiji la Dodoma ni pamoja na  Tanga ,songwe,Mwanza Moro,Arusha,Iringa na Mbeya ambao kwa pamoja wameeleza kuwa kwenye bajeti zao watahakikisha wanaelekeza kwenye maboresho ya maeneo ya machinga.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments