MASHIRIKA YANAYOTETEA HAKI ZA WAFUGAJI WAOMBA SERIKALI KUFANYA MAZUNGUMZO YA PAMOJA ILI KUMALIZA MGOGORO WA LOLIONDO SALE NA NGORONGORO


Katikati ni mkurugenzi wa mtandao wa wafugaji Tanzania( TPCF), Joseph Parsambei akitoa tamko la mashirika zaidi ya 20 juu ya mgogoro wa ardhi wilayani Ngorongoro.

Na Rose Jackson,ARUSHA

Zaidi ya Mashirika ishirini ya kiraia yanayotetea haki za wafugaji wa asili Tanzania wameiomba serikali na wananchi wilayani Ngorongoro kukaa kwa pamoja katika meza ya mazungumzo ili kumaliza mgogoro wa ardhi uliopo katika wilaya hiyo.

Akitoa tamko hilo kwa niaba ya mashirika hayo katika mkutano wa mashirika hayo ,Mkurugenzi wa Mtandao wa Wafugaji Tanzania ,Joseph Parsambei amesema kuwa wamekutana ili kufanya tathmini na kuelimishana juu ya mgogoro huo na namna ya kuutatua.

Amesema kuwa wao wakiwa kama mashirika ya kutetea haki za wafugaji wanaomba pande zote mbili kukaa kwa pamoja huku wakiomba mashirika hayo ya kiraia kuhusishwa ili waweze kutoa ushauri wao kwa kuwa nao ni sehemu ya jamii..

"Tumelazimika sisi mashirika kukutana kufanya tathmini ya mgogoro kutokana na taarifa wanazozisikia na kwamba wanatoa tamko katika eneo la Loliondo na Sale pamoja na mgogoro uliopo eneo la Ngorongoro na lengo letu ni kuomba meza huru iwepo ili kumaliza tatizo hili",aliongeza

Amesema kuwa wanatambua umuhimu wa uhifadhi na wanatambua haki za wananchi hivyo haki isikiukwe katika kutafuta uhifdhi.

Aidha amesema wanaunga mkono juhudi za kumaliza mgogoro huo huku kwa eneo la Loliondo Sale wanasisitiza kuwepo kwa matumizi sahihi ya ardhi kwani ndiyo suluhisho la mgogoro huo.

Parsambei ameomba kila upande uheshimu sheria za nchi haki za binadamu na utawala wa kisheria huku wakitaka wadau wote kujielekeza katika meza huru ya majadiliano ili kumaliza mgogoro bila kuchochea upande wowote.

Kwa upande wake Msaidizi wa Kisheria kutoka Shirika linalotoa msaada wa kisheria bi Agnes Marmo amesema kuwa wanaomba hatua zote zinazochukuliwa na serikali katika eneo la Loliondo Sale zishirikishwe kwa jamii husika ili kufikia muafaka .

Amesema kuwa kwa upande wa eneo la Loliondo Sale ni km za mraba elfu 1500 ambao mgogoro wake ni baina ya wananchi na wawekezaji huku mgogoro wa Ngorongoro ukiwa ni kati ya serikali na wananchi kwa madai ya ongezeko la watu na mifugo.

Aidha ameomba serikali na jamii kukaa meza huru ya majadiliano na wakubaliane na kwamba wadau wajikite katika mgogoro huo ili maslahi yote yalindwe.

Amesema wao kama mashirika ya utetezi wataendelea kuwa macho na karibu na sakata hilo ili kuhakikisha matumizi ya ardhi endelevu yanalindwa

Naye Afisa mipango kutoka Shirika la Masae Pastoralism Development Organization , Amani Sekilo amesema mgogoro wa tarafa ya Ngorongoro Ina sheria yak maalum hivyo kuna umuhimu sheria hiyo itumike vizuri kwani inatambua kuna wafugaji na uhifadhi.

Amedai kuwa Ngorongoro ni eneo la matumizi mseto na kwamba utatuzi wa migogoro hiyo na kwamba wao wanataka mbinu mbadala ya serikali kufanya mazungumzo ya pamoja ili wasiumizane.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments