MGONGOLWA : RAIS SAMIA AMEONESHA THAMANI HIFADHI ZA JAMII,VIONGOZI WAELEZENI WANANCHI

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Iringa Mjini, Joseph Mgongolwa amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuziagiza taasisi za Serikali zinazokopa mikopo chechefu kutoka mifuko ya jamii nchini zirejeshe mikopo hiyo.


Sambamba na kuwasilisha michango ya wafanyakazi katika mifuko hiyo kwa wakati ili iweze kutoa huduma bora kwa wanachama wake nchini.


Mgongolwa ametoa pongezi hizo leo Machi 30,2022 muda mfupi baada ya Rais Samia kupokea taarifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2020/2021 pamoja na ripoti ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino jijini Dodoma.


Mjumbe huyo amesema kuwa, hifadhi ya jamii ni mpango uliobuniwa tangu enzi na enzi kutoa ulinzi wa kijamii miongoni mwa wanajamii husika ili iweze kusonga mbele.


"Huu ni utaratibu wenye historia ndefu ikitajwa kuanza tangu zama za kale, historia inaonesha kuwa, enzi hizo binadamu walikuwa wakiishi katika makundi,makundi yaliyoundwa kwa lengo la kutoa ulinzi wa kiuchumi na kijamii kwa wanachama wake.


"Kutokana na changamoto zilizokuwa zinawakabili binadamu hao wa kale katika kujitafutia maendeleo, wanachama wa makundi hayo walikuwa wakisaidiana wao kwa wao kwa manufaa yao ya kimwili na kiuchumi.


"Makundi haya ya wanajamii yaliendelea kuwepo zama nyingi zilizofuatia mpaka pale Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) wa Desemba 10, 1948 ulipoasisi tamko lake mashuhuri la Azimio la Haki za Binadamu.


"Sehemu ya 22 ya azimio hili lilihitaji kila mtu katika jamii apatiwe ulinzi, huku likisisitiza,kila mwanachama wa jamii yoyote, ana haki ya hifadhi ya jamii kupitia juhudi za kitaifa na ushirikiano wa kimataifa (na) kulingana na mpangilio na rasilimali za kila nchi na hali za kisiasa na kiuchumi ya nchi husika.


"Aidha, kufuatia azimio hilo, Shirika la Kazi la Kimataifa (ILO) lilianzisha Sheria ya Hifadhi ya Jamii Namba 102 katika mkutano wake wa 35 mwaka 1952 na kubainisha angalau mafao tisa yaweze kutolewa na mifuko ya hifadhi ya jamii.Mfano mafao ya uzeeni, ulemavu, fao la warithi, majeruhi katika ajira, uzazi, afya, ugonjwa, kukosa ajira na kifo,"amefafanua.


Mgongolwa amesema, kwa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa wanaokopa katika mifuko hiyo warejeshe inadhihirisha kuwa, Serikali yake inathamini na kuheshimu sana hifadhi za jamii kutokana na faida lukuki zilizopo.


"Kila mmoja wetu, anatambua wazi kuwa,mifuko ya hifadhi ya jamii ni maalumu kwa ajili ya kumsaidia mfanyakazi kumudu mahitaji ya uzeeni pindi anapostaafu au mengine mengi, sababu kubwa iliyosababisha kuwepo mifuko ya hifadhi ya jamii ni baada ya kubainika kuwa, wakati wa ujana, wafanyakazi wengi hushindwa kujiwekea akiba ya kutosha kukidhi mahitaji ya uzeeni au kumudu gharama za maisha yao pindi itokeapo hali yoyote ya kutojiweza,"amesema.


Mgongolwa amefafanua kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia imejipambanua vilivyo kuhudumia wananchi na kuhakikisha kila mmoja anapata huduma bora wakiwemo wafanyakazi ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi.


Amesema, heshima ambayo Serikali inaendelea kuwapa watumishi na wafanyakazi nchini zikiwemo motisha zinatoa hamasa ya kufanya kazi kwa bidii, hivyo kuyafikia malengo ya Serikali kutoa huduma bora na hatimaye kupata maendeleo endelevu.


Wakati huo huo, Mgongolwa amesema kuwa, agizo la Rais Samia la kuwataka wabunge, mawaziri wanaosimamia kuwaambia ukweli wananchi kuwa vita ya Urusi na Ukraine vimepandisha bei ya mafuta linapaswa kuunngwa mkono na makada wote.


“Tumemsikia,Mheshimiwa Rais Samia amesema wazi kuwa, mafuta yanapopanda ndio kila kitu kinapanda, nauli zitapanda, usafirishaji wa bidhaa utapanda.


"Amesema, sasa hivi kutoa kontena la bidhaa kutoka China kuleta Tanzania, kwa kontena mfano la futi 40 lilokuwa dola za Marekani 1500 sasa hivi ni dola za Marekani 8,000 hadi 9,000. Hii inaonesha namna ambavyo, vita ile imechangia gharama za bidhaa, kwa msingi huo, makada,wanachama, viongozi wote tuwaeleze wananchi wetu kuhusiana na hali hii.


"Unapowapa taarifa sahihi kwa wakati wananchi, hii inaondoa hali ya maswali mengi ambayo wanayo, mfano bidhaa kama mafuta ya kula yapenda bei kwa kasi sana maeneo mengi duniani ikiwemo Tanzania, hii inachangiwa na mivutano au vita vinavyoendelea huko Ukraine,"amefafanua Mgongolwa.

 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post